Breaking

Monday 9 January 2023

MAJAMBAZI SUGU WANNE WATIWA MBARONI


Na lango la habari 

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kuwakamata Majambazi sugu wanne kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kihalifu vya unyang'anyi wa kutumia silaha.

Akithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao leo Jumatatu Januari 09, 2023 kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam ACP Muliro Jumanne Muliro amesema kuwa majambazi hao wamekamatwa tarehe 08/1/2023 majira ya saa 6 mchana eneo la Mabibo External Kinondoni.

Kamanda muliro amewataja majambazi hao kuwa  ni Athuman Yusuph Mbalilo maarufu Soti (50) Mkazi wa Kimara Temboni, Mpoki Raphael maarufu Mwangwisya (41) mkazi wa Mbezi luis na wengine wawili 

"Ukamataji huo ulitokana na taarifa fiche ya kuwepo kwa kundi hilo la kihalifu ambalo lilionekana kuanza kufanya matukio mbalimbali ya uhalifu wa kutumia silaha kuanzia tarehe 01/01/ 2023 hadi tarehe 07/1/2023 katika Jiji la Dar es Salam"

"Watuhumiwa hao wanne walikutana kupanga na kujiandaa eneo la kufanya uhalifu na walipobaini kuzingirwa na askari Polisi mmoja wao alitoa bastola yake na kupiga risasi kuwashambulia askari, na katika mazingira hayo askari haraka walijihami na kuwajeruhi watuhumiwa wote wanne kwa risasi na kufanikiwa kuwakamata" 

Kamanda Muliro amesema kuwa mahojiano ya awali na watuhumiwa hao na kumbukumbu za kihalifu za Polisi zimeonesha kuwa miongoni mwao waliwahi kukamatwa na kukaa kwenye mahabusu za Keko kwa tuhuma za mauaji na unyanganyi na walitoka 2017.

"mmoja wao akakimbilia nchi jirani na alirudi 2022 na kushiriki matukio yakiwemo jaribio la uporaji eneo la Mtaa wa Tandamti Kariakoo, kupora pesa huku wakitishia bunduki eneo la Kunduchi Mtongani, Goba walitishia silaha na kupora pesa, Keko, na Vikindu Wilaya ya Mkuranga pia walipora pesa" amesema kamanda Muliro

Watuhumiwa hao pia baada ya kukamatwa waliweza kuwaonesha askari bunduki aina ya AK 47 yenye namba za usajili UC 3889 1998 ikiwa na risasi 24 ndani ya Magazine, Bastola moja aina Star iliyofutwa namba ikiwa na Risasi nne (4) ndani ya magazini na zilikamatwa pia Pikipiki mbili aina ya Boxer nyeusi, MC 665 DMD na MC 475 DPH ambazo zimekuwa zikitumiwa kwenda na kutoka kwenye maeneo ya matukio yaliyotajwa.

Kutokana na majeraha waliyoyapata wakati askari wakijihami kwa risasi wahalifu hao walipelekwa hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu lakini hali zao sio nzuri. 

Juhudi za kuwatafuta majambazi wengine ambao hawajakamatwa zinaendelea na lazima watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vingine vya kisheria.

Kamanda Muliro amesema kuwa Jeshi la Polisi linachukizwa sana na halitavumilia hata kidogo kuona wahalifu wakiwasumbua wananchi kwa vitendo vya kihalifu.

"Jeshi halitakuwa na hururna lakini litazingatia sheria kuwashughulikia kwa haraka sana kila atakaye jihusisha au kutenda vitendo vya ovyo vya kihalifu"

"Jeshi la Polisi litaendelea kutimiza majukumu yake na kuhakikisha usalarna unaimarika zaidi na hakutakuwa na mwanya wawahalifu kulazimisha kurudi tulikotoka." Amesisitiza Kamanda Muliro

 Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za kihalifu na wahalifu na kuahidi kuwa Jeshi la Polisi litazitunza na kuzifanyia kazi haraka iwezekanavyo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages