Breaking

Tuesday 10 January 2023

TABORA WAKUNWA NA UTENDAJI WA RAIS SAMIA



Na Lucas Raphael,Tabora

Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini Emanuel Adamson Mwakasaka alimshukuru Rais kwa kuwaongezea bajeti Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) hali iliyopelekea barabara na madaraja kutengenezwa katika kata zote.

Wakiongea kwa nyakati tofauti katika kikao cha bajeti cha baraza hilo kilichofanyika juzi katika ukumbi wa mikutano wa manispaa hiyo walisema serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Samia imewatendea haki wananchi.

Mwakasaka alisema kwamba serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA)imefanikiwa kupata fedha za kutosha za kuhakikisha barabara za manispaa hiyo zinapitika muda wote wa mwaka.

Ili miundombinu hiyo idumu alishauri watendaji wa vijiji na kata kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi kuhakikisha magari yenye uzito mkubwa hayapitishwi katika madaraja na barabara hizo na ikibidi ziwekwe alama za uzito wa magari.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ramadhan Kapela alisema kwamba madiwani wa halmashauri ya manispaa Tabora wanampongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kasi kubwa ya utekelezaji miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Alibainisha kuwa miradi mingi katika manispaa hiyo ilikuwa inasuasua kutokana na ufinyu wa bajeti lakini baada ya kuingia madarakani Rais amemwaga fedha katika sekta zote ikiwemo elimu, afya, barabara, maji na nyinginezo hivyo kuongeza kasi ya utekelezaji miradi ya maendeleo katika sekta hizo.

Ramadhan alisema Rais Samia kila siku anafanya jambo jipya linalogusa maisha ya wananchi hali inayopelekea kutatuliwa kero zao.

Aliongeza kuwa halmashauri hiyo haijawahi kupata asilimia 100 ya makadirio ya bajeti yake ya maendeleo lakini chini ya uongozi wa Rais Samia wameletewa fedha zote walizoomba na kufanikisha utekelezaji mipango yao ya maendeleo.

‘Tunamkushukuru sana Rais kwa kutuletea zaidi ya bil 1.5 za ujenzi wa hospitali ya wilaya huduma sasa zinatolewa, pia sh bil 1 kwa ajili ya jengo la utawala na kila mwezi anatuletea fedha za mfuko wa Jimbo na za matumizi mengineyo’, alisema Ramadhan.

Aidha alipongeza hatua ya Rais Samia kuanza kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima kwa kuwapunguzia gharama kutoka sh 140,000 hadi sh 70,000 tu kwa mfuko wa mbolea na kubainisha kuwa itawasaidia kuongeza uzalishaji mazao yao.

Kaimu Mkurugenzi wa manispaa hiyo Seif Salumu alisema wataendelea kusimamia utekelezaji miradi yote kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha thamani ya fedha (value for money) inaonekana ili kuwanufaisha wananchi.

Mwisho.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages