Breaking

Monday 30 January 2023

TAWA WAJENGA MADARASA, OFISI YA WALIMU USINGE



Na Lucas Raphael,Tabora

MAMLAKA ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujenga vyumba 2 vya madarasa na ofisi 1 ya walimu katika shule ya msingi Usinge wilayani Kaliua Mkoani Tabora .

Akikabidhi madarasa hayo jana kwa niaba ya Meneja wa Mamlaka hiyo Kanda ya Magharibi, Kamanda wa Pori la Akiba la Moyowosi Daud Mnyampwani alisema mradi huo umegharimu jumla ya sh mil 50.

Alibainisha kuwa wamejenga madarasa hayo ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha watoto wote walioandikishwa kuanza darasa la kwanza wanapata nafasi katika shule hiyo.

Aliongeza kuwa Mamlaka hiyo imekuwa ikifadhili miradi ya maendeleo katika Mikoa na Wilaya mbalimbali ili kuwezesha jamii kupata huduma stahiki katika maeneo yao.

‘Tutaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya jamii, tunaomba wananchi waendelee kutupa ushirikiano kwa kuacha kuvamia mapori ya hifadhi za serikali ili kulinda uoto wa asili’, alisema.

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Michael Nyahinga aliishukuru Mamlaka hiyo kwa kuwa mdau mzuri wa maendeleo ya wananchi katika wilaya hiyo na kuomba wadau wengine kuiga mfano huo.

Aliwataka walimu na wanafunzi wa shule hiyo kutumia vizuri vyumba hivyo ili viwe chachu ya kuongeza ufaulu wao na kuwawezesha kutimiza malengo yao ya kitaaluma.

Aidha aliiomba TAWA kuendelea kusaidia jamii kwa kutekeleza miradi mbalimbali ili kupunguza kero za wananchi katika sekta za afya, maji na nyinginezo.


Mwisho.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages