Breaking

Monday 13 February 2023

WAKILI AFARIKI HOTELINI BAADA YA KUNYWA DAWA ZA KUONGEZA NGUVU ZA KIUME



Wakili maarufu mtaani Kitengela, kaunti ya Kajiado nchini Kenya amefariki dunia baada ya kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, iliripotiwa kwamba wakili huyo mwenye umri wa miaka 52, alianguka na kuzirai katika hoteli mtaani humo na kukimbizwa hospitalini ambapo alithibitishwa kufariki.

“Mkurugenzi wa hoteli hiyo akiwa ameambatana na meneja walitoa taarifa kuwa majira ya saa 7:30 usiku wa kuamkia Ijumaa, Februari 10, wakili alizirai katika hoteli hiyo mtaani Kitengela na kukimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan, tawi la Kitengela ambako alithibitishwa kufariki alipowasili," ilisoma sehemu ya ripoti ya polisi.

Maafisa wa polisi na makachero wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) walifika eneo la tukio na kubaini kuwa marehemu akiwa kwenye mgahawa huo, alimeza tembe za dawa zinazoaminika kuwa za kuongeza nguvu za kiume.

"Alikuwa na mwanamke mmoja anayeaminika kuwa mpenzi wake, na karani katika kampuni hiyo ya mawakili. Hapo awali alikuwa amepanga chumba katika hoteli hiyo kwa usiku huo," ripoti hiyo iliongeza.

Ripoti hiyo pia iliongeza kuwa polisi walipata tembe aina ya Ascard 75 ambayo hutumika kutibu shinikizo la damu.

"Mke wake alithibitisha kuwa ana shinikizo la damu. Hakukuwa na majeraha yoyote mwilini," ripoti ya polisi iliongeza.

Mwili wa marehemu ulihamishwa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee Funeral Home ukisubiri uchunguzi wa maiti.

Via: Tuko News
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages