Breaking

Thursday 23 February 2023

WATOTO 101,398 TABORA WAANDIKISHWA DARASA LA KWANZA



Na Lucas Raphael,Tabora

MKOA wa Tabora umefanikiwa kuandikisha jumla ya watoto 101,398 wa darasa la kwanza mwaka huu 2023 na kuvuka lengo lililowekwa awali kwa zaidi ya asilimia 108.8.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Batilda Burian alipokuwa akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika jana katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi mjini hapa.

Alisema idadi ya watoto wanaoandikishwa kuanza darasa la kwanza imekuwa ikiongezeka kila mwaka katika wilaya zote za Mkoa huo na kwa mwaka huu wamevunja rekodi zaidi.

Balozi Batilda alisema hadi kufikia Februari 2023 jumla ya watoto 101,398 wa darasa la kwanza wameripori shuleni ambao ni zaidi ya asilimia 108.8 ya lengo na watoto 38,575 sawa na asilimia 83.8 ya waliochaguliwa wameanza kidato cha 1.

Alibainisha kuwa mwitikio huo umetokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo ujenzi wa shule mpya.

‘Tunamshukuru sana Mhesh.Rais kwa kutuletea sh bil 11.3 mwezi Oktoba 2022 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 565 katika shule zote ili kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kuingia kidato cha 1 wanapata nafasi’, alisema.

Alimshukuru Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt John Mboya, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri na Maofisa Elimu kwa kusimamia kwa weledi mkubwa ujenzi wa madarasa hayo.

Aliwataka kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanaripoti na wale ambao hawajaripoti katika shule walizopangiwa wasakwe kokote walipo ili wasipoteze fursa hiyo.

Balozi Batilda alifafanua kuwa tangu Rais Samia aingie madarakani hadi sasa ameshatoa zaidi ya sh bil 48 kwa Mkoa huo kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya kutolea huduma za eimu katika shule za msingi na sekondari.

Alisema kupitia fedha hizo wameweza kujenga shule mpya 12, vyumba vya madarasa 2,549, mabweni 6, maabara 3, mabwalo ya chakula 3 na matundu ya vyoo 250, na sh bil 41.7 zimetumika katika utoaji elimu bila malipo.

Mwisho.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages