Breaking

Saturday 11 February 2023

WAZIRI UMMY ASISITIZA UADILIFU UTOAJI HAKI UPIMAJI VINASABA



Na WAF- DOM

WAZIRI wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ametoa wito kwa Watumishi wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa waadilifu na utendaji wa haki katika kuwahudumia wananchi wanaofika katika mamlaka hiyo hususan wanakuja kupata huduma za kupima vinasaba.

Waziri Ummy amesema hayo, wakati alipofanya ziara ya uzinduzi wa jengo la ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kuongea na Watumishi katika ofisi hizo zilizopo Jijini Dodoma.

Amesema, "Kazi yenu hii inauhusiano wa karibu na mambo ya kutenda haki, na mimi kwasababu ni mwanamke, kwahiyo katika swala la kuchunguza uhalali wa baba wa mtoto ni yupi napenda sana tuwe waadilifu ili kutenda haki ya kweli bila kuonea yoyote."

Sambamba na hilo, Waziri Ummy ameelekeza Taasisi zote za umma na binafsi kutenga vyumba na mabafu kwaajili ya watumishi wao kufanya mazoezi ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupambana dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Ameendelea kusema kuwa, kama nchi inaendelea kushuhudia ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo kisukari, saratani, magonjwa ya moyo na afya ya akili ambayo yanaweza kudhibitika endapo maelekezo ya kitaalamu yatafuatwa.

Aidha, amewaelekeza Wataalamu wa Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali kutoweka vikwazo kwa Waganga wa tiba asili pindi wanapopeleka dawa zao kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi ili kufahamu endapo dawa hizo zina kemikali inayoweza kudhuru mwili wa mwanadamu au hazina.

Pamoja na hayo, Waziri Ummy ameelekeza Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali kukaa pamoja na Bandari ili kuweka sawa namna ya upokeaji wa bidhaa na kemikali ili zisiingiliane kwa lengo la kuboresha usalama wa bidhaa zote zinazoingia nchini kupitia bandari.

Nae, Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko amesema, kukamilika kwa ujenzi wa jengo la Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali kutasaidia kusogeza huduma za kutosha kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali hasa katika mikoa ya mbali iliyokuwa ikipata huduma hizi Jijini Dar es Salaam.

Sambamba na hilo, Dkt. Mafumiko ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kusaidia bajeti ya upatikanaji wa vifaa vitavyosimikwa katika maabara hiyo ili ianze kutoa huduma kwa haraka, huku akisisitiza tayari Mamlaka hiyo imeanza kutenga fedha za ununuzi wa baadhi ya vifaa hivyo.

Mwisho.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages