Breaking

Tuesday, 7 March 2023

AJALI YA BASI YAUA WATU TISA, YAJERUHI 30 KATAVI

Watu tisa wamepoteza maisha na wengine 30 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Kombas kuacha njia na kupinduka kwenye korongo la mlima Nkondwe wilayani Tanganyika.


Ajali hiyo imetokea jana Machi 6 saa 9:45 alasiri ambapo imeelezwa kuwa baada ya kufika eneo la mlima Nkondwe basi hilo liliserereka hadi kwenye korongo hilo lenye kina cha mita zisizopungua 75 chini yake kukiwa na mto.


Mganga Mkuu hospitali ya wilaya ya Tanganyika Daktari Alex Mrema amesema vifo hivyo vimetokea papo hapo, ambapo wanaume walikuwa watano kati yao kulikuwa na mtoto mmoja anayekadiriwa kuwa na umri miaka miwili.


"Wanawake wanne pia wamepoteza maisha wote watu wazima kati ya umri wa miaka 18 hadi 22 na mmoja mwenye umri kati ya 30 hadi 35 mwingine alikuwa mjamzito," amesema Mrema.


Aidha amesema kati ya majeruhi 30, baadhi yao wamepokelewa hospitalini hapo na wengine wanne wamepelekwa hospitali ya rufaa mkoa wa Katavi huku wengine wakitibiwa na kuondoka.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ally Makame amethibitisha kutokea tukio hilo na kwamba wanaendelea kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.


"Lakini tunatoa nasaha kwa madereva wetu kuwa makini na kuchukua tafadhari kubwa sana wanapopita kwenye milima hatarishi kama huu wa Nkondwe ni hatari mkoani kwetu," amesema Makame.Via: Mwananchi

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages