Breaking

Wednesday, 8 March 2023

AJALI YAUA WATU NANE, YAJERUHI 49 GEITAIdadi ya waliofariki katika ajali ya Basi la Sheraton lililokuwa likifanya safari zake kutoka jijini Mwanza kwenda Ushirombo mkoani Geita iliyotokea jana Machi 7, 2023 katika eneo la Ibandakona wilayani Geita, imeongezeka na kufikia watu wanane baada ya mmoja kupoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Geita, Dk Mfaume Salum akizungumza na mwananchi asubuhi ya leo amesema majeruhi mmoja kati ya 50 waliokuwa wamefikishwa hospitalini hapo alifariki dunia wakati madaktari wakijitahidi kuokoa maisha yake.


Dk Salum amesema hadi sasa majeruhi walioko hospitalini hapo ni 49 ambapo wanaume ni 25 na wanawake 24 na waliofariki papo hapo kwenye ajali ni watu saba kati yao wanawake ni wanne na wanaume watatu pamoja na majeruhi mmoja aliyefariki wakati akipatiwa matibabu.Amesema majeruhi wanne ambao hali zao hazikuwa nzuri wamepewa rufaa kupelekwa Hospitali ya Kanda Bugando  kwa matibabu zaidi.


Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Berthaneema Mlay amesema chanzo cha ajali ni tairi ya mbele ya gari kupasuka na kusababisha gari kutumbukia kwenye korongo na kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha dereva alikuwa kwenye mwendo wa kasi.


Chanzo: Mwananchi

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages