Breaking

Wednesday 1 March 2023

SUNGUSUNGU WATANO KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA MAUAJI

Na Lucas Raphael,Tabora


WALINZI wa jadi 5 maarufu kwa jina la Sungusungu Wilayani Sikonge Mkoani hapa wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Tabora kwa tuhuma za mauaji ya Abdallah Idd wakiwa kwenye doria.

Awali akisoma mshitaka Wakili upande wa Jamhuri Joseph Makene mbele ya hakimu mkazi John Mdoe aliambaia mahakama hiyo kwamba watuhumiwa wote 5 wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya kusudia katika Kijiji hicho Aprili 14 mwaka jana.

Wakili huyo aiwataja waliopandishwa kizimbani kuwa ni  Kamanda wa kikundi hicho cha Sungusungu Bakari Kiyola, Mrisho Maulid, Mashaka Christopher, Kassim Christopher na Jamila Ibrahim.

Aliiambia mahakama kuwa ushahidi wa shauri hilo umekamilika na upande wa Jamhuri utaleta mashahidi 10 na vielelezo 2 ambavyo ni taarifa ya Daktari na ramani ya eneo ulipotupwa mwili wa marehemu baada ya kuteswa walipokuwa wakimhoji kuhusiana na tukio la kuvunjwa vibanda vya maduka.

Hakimu Mdoe alipowahoji washtakiwa kama watakuwa na mashahidi, mshtakiwa namba 1 Bakari Kiyola yeye alisema hana shahidi yoyote huku wenzake wanne wakisema kuwa watakuja na mashahidi wawili wawili kila mmoja.

Washitakiwa wote 5 walirejeshwa mahabusu kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo kisheria kusikiliza shauri hilo la mauaji.

Alieleza kuwa watasubiri hadi Msajili wa Mahakama atakapopanga tarehe ya kuanza kusikilizwa shauri lao katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na kutolewa uamuzi.

Ilielezwa kuwa kipigo hicho kilitokana na kijana huyo kupigiwa kura za ndiyo na wananchi kuwa anahusika kwenye tukio la kuvunja na kuiba kwenye vibanda vya maduka kijijini hapo.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages