Breaking

Saturday 4 March 2023

WANANCHI WAISHIO PEMBEZONI MWA VYANZO VYA MAJI KIBAHA WAPATA ELIMU



Na Fredy Mshiu

Wananchi wa Kijiji Cha Minazi Mikinda  Kitongoji cha Lubungo Wilaya ya Kibaha Vijijini wameelimishwa juu ya umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji (Mto Ruvu) kutoka kwa Watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kwa kushirikiana na Bonde la Wami Ruvu.


Elimu iliyotolewa imehusisha kuwahasa wananchi kuacha tabia ya kufanya kilimo katika vyanzo vya maji, uchimbaji wa madini katika vyanzo, pamoja na kuingiza makundi ya mifugo katika vyanzo vya maji.


Akiongea na wananchi wa Vitongoji hivyo Mhandisi wa Mazingira DAWASA ndugu, Sophy Ayoub  amewataka wananchi kuacha haraka uharibifu wa vyanzo vya maji kwani ni hatari kwa sasa na vizazi vijavyo.


"Uharibifu wa vyanzo vya maji huchangia kwa kiasi kikubwa mto kukauka, kuingiza mifugo na kilimo katika vyanzo vya maji kunapelekea mabadiliko ya tabia ya nchi yanayoleta ukame wa muda mrefu na maji kukauka katika vyanzo" ameeleza ndugu Sophy.


Sambamba na hayo wananchi wa Kijiji Cha Minazi Mikinda wameelimishwa juu ya Sheria ya utunzaji wa Mazingira na vyanzo vya maji na wapi mahali sahihi wanapaswa kufanya shughuli za kilimo pamoja na ufugaji kutoka kilipo chanzo cha maji.


Ndugu, Yulian Mizola Afisa Maendeleo kwa jamii kutoka Bonde la Wami Ruvu ameyaasa makundi yote yanayohusika na uharibifu wa Mazingira katika mto Ruvu kuwa Sheria haitabagua mtu yeyote anayehusika na uharibifu wa vyanzo vya maji na adhabu Kali zitachukuliwa juu yao.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Lubungo ndugu, Selemani Mgweno ameshukuru DAWASA pamoja na Bonde la Wami Ruvu kwa kuleta elimu hii kwa wananchi wa eneo lake ambao wengi ni wafugajj na wakulima.


"Elimu mnayotupatia Leo hii ni muhimu sana, sasa wananchi watakua na uwezo wa kutambua ni wapi wanastahili kufanya shughuli zao za ufugaji na kilimo Ili wasilete athari za kimazingira na kuharibi vyanzo vya maji"ameeleza ndugu Mgweno


Wananchi wa Kijiji Cha Minazi Mikinda wameonyesha utayari wa kuacha kufanya shughuli za kijamii katika vyanzo vya maji huku wakiahidi kuwa mabalozi kwa wenzao wengi juu ya ulinzi wa vyanzo vya maji.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages