Breaking

Tuesday 30 May 2023

MABORESHO BANDARI YA DAR ES SALAAM YAZAA MATUNDA , UWEZO KUHUDUMIA SHEHENA WAONGEZEKA

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI wa Bandari ya Dar es Salaam Mrisho Mrisho amesema bandari hiyo imepita katika hatua mbalimbali za maboresho lengo likiwa kuongeza ufanisi ikiwemo kuhudumia shehena zinazoingia na kutoka kwenye bandarini hapo.

Aidha amesema kutokana na maboresho makubwa ambayo yamefanyika yamewezesha bandari hiyo hadi kufikia Mei mwaka huu kuhudumia shehena ya mzigo zaidi ya tani milioni 18 kutoka kwenye lengo lililowekwa la kuhudumia tani milioni 19.6 .

Akizungumza leo na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, Mrisho ameeleza kwamba baada ya kufanyika kwa maboresho, utendaji kazi umeongezeka na upo uwezekano kwa muda uliobaki kuvuka lengo hadi kufikia kuhudumia tani milioni 20 za shehena na hivyo itakuwa imeweka historia.

"Maboresho ambayo yamefanyika ni pamoja na kuongeza kina cha maji ambacho kimeongezeka kutoka mita 6-7 hadi kufikia mita 14.5 na kuwezesha meli kuhudumiwa katika gati lolote ndani ya bandari ya Dar es Salaam". Amesema

Amefafanua hatua hiyo imefanya kuwa na idadi kubwa ya meli zinazohudumiwa katika bandari hiyo na kuongeza maboresho mengine ni ujenzi wa gati mpya tatu (03) na kuboresha magati yaliyokuwepo awali.

Mrisho amesema moja ya matokeo chanya yaliyoonekana ni pamoja kuongezeka kwa idadi kubwa ya meli kubwa (Deep sea vessel) zaidi ya 90 kuhudumiwa ndani ya mwezi mmoja.

Ameongeza kwa sasa hata wanaotumia bandari ya Dar es Salaam wameongezeka kwani kwa mwaka mmoja wanahudumia magari kati ya 250,000 hadi 300,000, na asilimia 60 ya magari hayo ni ya nchi jirani.

Pamoja na hayo ameeleza kwa sasa katika bandari hiyo kuna gati jipya linalohudumia shehena ya magari jambo ambalo limeifanya bandari hiyo kuweka rekodi ya kihistoria kwani hapo awali shehena ya magari ilikuwa ikihudumiwa kwa kuchanganywa na shehena nyingine.

Kuhusu dhana ya ushiriki wa sekta binafsi amesema ni lazima kuwe na ushiriki wa sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari, na hiyo inafanyika duniani kote.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Uwakala ya Epic Mhandisi Tonny Swai ambaye ni miongoni mwa wadau wakubwa wa bandari hiyo amewaomba watanzania kutumia bandari hiyo ambayo ni salama.

Pamoja na hayo waandishi waliotembelea bandari hiyo wameelezwa imekuwa ni lango la kuu la kibiashara, asilimia 95 ya biashara ya kimataifa ya Tanzania inahudumiwa na bandari hiyo.
Matukio mbalimbali katika picha yakimuonesha Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho akielezea utendaji kazi wa sehemu mbalimbali za bandari hiyo.

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari ofisini kwake leo Mei 29, 2023

Mdau wa Bandari ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwakala ya Epic, Mhandisi Tonny Swai akiwaelezea waandishi wa habari hali ya utendaji kazi wa bandari ya Dar es Salaam baada ya maboresho makubwa yaliyofanyika katika bandari hiyo
Mwonekano wa baadhi ya maboresho yaliyofanywa katika bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji huduma








Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages