Breaking

Saturday 20 May 2023

PROF. BISANDA: UMRI SI KIKWAZO KUPATA ELIMU


Jamii ya Watanzania imetakiwa kuachana na dhana ya kuwa umri ukisogea basi hakuna tena fursa ya kujiendeleza katika elimu ya juu.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Prof. Elifas Bisanda, alipotembelea banda la maonesho la chuo hiki May 19, 2023 katika maonesho ya pili ya Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) yanayoendelea katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

“Dhana ya kusema kuwa ukiwa mzee huwezi tena kupata nafasi ya kusoma elimu ya juu kwa sasa imepitwa na wakati, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania tunatoa fursa kwa marika yote bila kubagua umri na shughuli zao haziwezi kufa au kusimama kwa sababu zozote za kishule kwani wanasoma na huku wanaendelea na shughuli zao za kila siku.” Amesema Prof. Bisanda.

Aidha, alisisitiza kuwa kinachoangaliwa katika kujiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni ukamilifu wa vigezo vinavyotakiwa katika kujiunga na elimu ya juu pekee kwani kwa mfumo wa elimu hii hata asiyeweza kujongea anaweza kumudu kusoma.

Akithibitisha hilo, mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika programu ya msingi (Foundation Program), Ndg. Felix Ringo, mwenye umri wa miaka 55 licha ya kuwa umri wake umesonga na kubanwa na majukumu mengi ya kimaisha bado ameweza kujiunga na chuo hiki na dhamira yake ni kufika mbali kitaaluma katika umri huo.

“Kwa umri huu nilionao nimebanwa na mambo mengi nisingeweza kujiendeleza kupitia elimu za kukaa darasani, kupitia chuo Kikuu Huria cha Tanzania nimepata fursa adhimu kabisa na nina shauku kubwa ya kusoma hadi kufikia ngazi za juu za usomi. Nimeanza mwaka huu na ninajiandaa na mitihani ya majaribio hivi karibuni.” Amesema Ndg. Ringo.

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko, Dkt. Mohamed Maguo, amefafanua kuwa dhima halisi ya uanzishwaji wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ilikuwa ni kuwainua kielimu watumishi na watu waliokosa fursa ya kuhudhuria elimu za darasani kutokana na kubanwa na majukumu mbalimbali ya kimaisha. Hivyo, hata wale wanaohisi umri wao umeanza kuwatupa mkono, chuo hiki ni sehemu pekee yenye fursa ya wao kupata elimu ya juu ambayo wanahisi walishaipoteza.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages