Breaking

Thursday 15 June 2023

MADINI MKAKATI YAJADILIWA MKUTANO WA 9 WA EITI



Dakar, Senegal 


Mkutano wa Kimataifa wa Asasi ya Kimataifa ya Uwazi na Uwajibikaji (EITI - Extractive Industry Transparency Initiative) uliofanyika Jijini Dakar nchini Senegal  kuanzia tarehe 13 -14 Juni 2023 umejadili fursa mbalimbali  kwenye Sekta ya Madini ikiwemo namna nchi zenye utajiri wa Madini Mkakati zinavyoweza kuzalisha Madini hayo kwa kuzingatia vigezo vya Uwazi na Uwajibikaji ili kuhakikisha kuwa Madini hayo yanawanufaisha wananchi wa maeneo yanapozalishwa na kuchangia katika kuinua uchumi wa mataifa husika.


Akichangia hoja katika mkutano huo,  Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa alisema Tanzania ina aina nyingi za Madini mkakati yakiwemo Nikeli, Graphite (Kinywe), Rare Earth Elements, Cobalt, Lithium, Manganese, Vanadium, Niobium, Titanium, Tin, na Copper (Shaba). 


Aliongeza kuwa, Madini hayo yanahitajika kwa wingi duniani kwa sasa na hivyo kinachohitajika zaidi ni ushirikiano (Partnerships) kati ya Serikali na wawekezaji mahiri kwenye masuala ya utafiti wa kina, uchimbaji wa kisasa, na uchakataji wa bidhaa za ndani na kuyaongeza thamani Madini ndani ya nchi suala ambalo litaongeza tija na kutoa fursa za ajira kwa wazawa na  kukuza biashara ya bidhaa za Madini yaliyoongezwa thamani kwa walaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi. 


Aidha, katika mkutano huo, mada mbalimbali zilijadiliwa kwa siku mbili ikiwa ni pamoja na masuala ya vipaumbele katika Uwajibikaji na Uwekaji wazi kumbukumbu za uzalishaji na biashara ya Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia katika kipindi cha miaka kumi ijayo; uwekaji wazi Mikataba kati ya Serikali na wawekezaji; uwekaji wazi takwimu za wenye hisa katika kampuni za uwekezaji; sambamba na kujadili mbinu za kukabiliana na rushwa na ufisadi katika Sekta za Madini, mafuta na Gesi Asilia.


Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na washiriki kutoka nchi zipatazo 90 ulihitimishwa Juni 14, 2023.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages