Breaking

Monday 5 June 2023

NHIF YAELEKEZWA KUTOA HUDUMA HADI NGAZI YA ZAHANATINA MWANDISHI WETU, WAF Dodoma

NAIBU Waziri wa Afya, Dkt.Godwin Mollel ameelekeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHF) kutoa huduma mpaka ngazi ya zahanati kwa vituo vyote vilivyokidhi vigezo vya kupewa huduma hiyo, ikiwemo kigezo cha kusajiliwa.

Dkt. Mollel ametoa maelekezo hayo leo Juni 5, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Mhe. Husna Juma Sekiboko katika Bunge la 12 Mkutano wa 11 kikao cha 40 jijini Dodoma. 

"Nawaagiza Bima ya Afya wapitie nchi nzima wahakikishe vituo vyote ambavyo vimetimiza hivi vigezo, ikiwemo kigezo cha kusajiliwa viingizwe na kuanza kutoa huduma hiyo,"Amesema Dkt. Mollel. 

Amesema, katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora katika vituo vyote vya kutolea huduma, tayari Serikali kupitia Wizara ya Afya imeagiza vifaa na vifaa tiba ambavyo vitasambazwa katika vituo mbalimbali nchini.

Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, katika kuongeza huduma za dawa zinazotolewa na bima katika zahanati na vituo vya afya Wizara imeongeza idadi ya dawa, vifaa na vifaa tiba ngazi ya Zahanati kutoka aina 254 mwaka 2015 hadi kufikia aina 451 mwaka 2023.

Ameendelea kusema kuwa, idadi ya dawa, vifaa na vifaa tiba ngazi ya Kituo cha Afya kutoka aina 414 mwaka 2015 hadi kufikia aina 828 mwaka 2023 huku akisisitiza dawa zilizoongezeka zipo katika miongozo ya Serikali na hivyo hulipiwa na Bima ya Afya kwa wanufaika wa mfuko. 

Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema katika kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa dawa za kisukari na shinikizo la damu inatatuliwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeongeza bajeti ya ununuzi wa dawa utaosaidia kusambaza dawa hizo nchi nzima mpaka katika ngazi ya zahanati. 
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages