Breaking

Thursday 13 July 2023

MAAFISA UTUMISHI WATAKIWA KUWA WABUNIFU UTENDAJI KAZINa Mwandishi Wetu - Kisarawe

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Maafisa Utumishi nchini kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa maendeleo ya taifa.

Mhe. Kikwete amesema hayo Julai 12, 2023 alipokuwa akizungumza na watumishi wa Umma Mkoa wa Pwani, Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma mkoani humo.

“Nataka kusikia kila Afisa Utumishi anajiwekea ratiba ya kuzungumza na watumishi anaowasimamia ili kusikiliza maoni, malalamiko au changamoto zozote wanazokutana nazo kwa lengo la kuboresha utumishi wa umma nchini utakaoweza kuwahudumia wananchi kikamilifu,” amesema Mhe. Kikwete.

Aidha, Mhe. Kikwete amewataka Maafisa Utumishi kuweka utaratibu wa kujua mahitaji ya watumishi kwa kuzingatia hali halisi ili kukidhi haja mbalimbali za watumishi bila kuwa na malalamiko.

Mhe. Kikwete amesema kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka Maafisa Utumishi hao kuwa wasemaji wa watumishi wanaowasimamia na kutatua kero na changamoto zao.

Mhe. Kikwete amewasihi watumishi wa umma kuendelea kufanya kazi kwa juhudi, werevu na weledi mkubwa katika kuwatumikia wananchi

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Bw. Baptista Kihanza ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kupata rasilimaliwatu ambayo imesaidia kupunguza tataizo la uhaba wa watumishi katika halmashauri hiyo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete anaendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa wa Pwani ikiwa ni siku ya tatu akilenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF katika mkoa huo ambapo leo alikuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages