Breaking

Tuesday 19 September 2023

NJOMBE YAONGOZA KWA IDADI KUBWA YA MADINI MKAKATI



Utafiti wa awali uliofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ulibaini kuwa Mkoa wa Njombe unaongoza kuwa na idadi kubwa ya Madini Mkakati kati ya Mikoa yote nchini.

Hayo yameelezwa na Meneja wa Sehemu ya Jiolojia kutoka GST Maswi Solomon baada ya kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka kwa lengo la kuwasilisha Vitabu vinavyoonesha Madini yapatikanayo Tanzania.

Mtaka amesema Mkoa wa Njombe una jumla ya Wilaya nne ambazo ni Njombe, Makete, Ludewa na Wanging'ombe ambapo Kitabu hicho kitawasaidia wananchi wa Mkoa huo na Wilaya zake kuvutia Wawekezaji Mkoani humo.

Aidha, ametoa wito kwa GST kutumia uzoefu walionao kwenye madini yaliyozoeleka nchini na kuupeleka kwenye Madini Mkakati ili kuepuka changamoto na migogoro iliyotokea huko nyuma hususan kwenye madini ya dhahabu.

Pia, Mtaka ameipongeza GST kwa kuchora Ramani za Madini nchi nzima na kuishauri taasisi hiyo kuendelea kufanya tafiti za madini, maji na nishati katika maeneo mbalimbali nchini.


Kwa upande wake, Meneja wa Sehemu ya Jiolojia kutoka GST Maswi Solomon amesema kufuatia uwepo wa Madini mengi ya kimkakati katika Mkoa wa Njombe Kitabu hicho kitasaidia kutambua aina ya madini yaliyopo na kusaidia kuvutia Wawekezaji Mkoani humo ili kufanya utafiti wa kina kwa kuwa utafiti wa kina na uvunaji wa madini mkakati huhitaji teknolojia ya juu ambayo wachimbaji wadogo wanashindwa kumudu gharama zake.

Pamoja na Mambo mengine, Maswi ametaja baadhi ya Madini Mkakati yaliyopo Mkoani humo ambapo ni pamoja na chuma, makaa ya mawe, titanium, vanadium, chromium, PGM, REE, shaba, Manganese, gesi ya methane na dhahabu.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages