Breaking

Tuesday 19 September 2023

DKT. BITEKO AZITAKA KAMPUNI ZA BIMA KUTOA ELIMU KWA UMMA KUHUSU FAIDA ZA BIMA

 

Na Timotheo Mathayo, Dar es Salaam.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amezitaka kampuni za Bima nchini kuendelea kutoa elimu kwa umma ili kuwajengea uwezo Wananchi kufahamu faida ya kuwa na bima zitakazowasaidia katika nyanja mbalimbali ikiwemo makazi na usafiri.

Dkt. Biteko ameyasema hayo leo tarehe 19 Septemba, 2023 wakati akizungumza na Watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) katika Ofisi ndogo za Wizara ya Nishati Jijini Dar  es Salaam.

"Elimu ya bima kwa wananchi bado haijaeleweka vizuri, hivyo nendeni mkatoe elimu ili wananchi wapate mwamko wa kukata Bima ya rasilimali zao, msijikite kwenye kutafuta masoko tu," amesema Dkt. Biteko.

Amefafanua kuwa ili kuendelea kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla, kampuni za Bima zinatakiwa kutunza fedha zake kwenye Benki za ndani ya nchi jambo ambalo litachochea  maendeleo.

Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Katibu Mkuu Kiongozi Mha. Zena Ahmed Said ambaye pia ni Balozi wa Bima Tanzania amesema Mamlaka inaendelea na mkakati wa kutoa elimu kwa umma kwa kushirikiana na mashirika ya Serikali na Sekta Binafsi.

Amesema kuwa, lengo ni kuwafikia  watanzania asilimia 80 wenye zaidi ya umri wa miaka 18 ifikapo mwaka 2030 pia  Mamlaka inaendelea na hatua ya  kuhamasisha Wizara na Taasisi za Serikali ziweke Bima kwenye miradi inayotekelezwa katika Sekta hizo.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba pamoja na Mabalozi wa Bima nchini.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages