Breaking

Thursday 14 September 2023

SEKTA YA MADINI KUFUNGAMANISHA SEKTA NYINGINE KIUCHUMI KUPITIA TAARIFA ZA MIAMBA






Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa Sekta ya Madini inatarajiwa kuwa chanzo cha taarifa sahihi za Miamba itakayosaidia kuendeleza sekta zingine ikiwemo ya Kilimo na Viwanda na hatimaye kujenga uchumi wa Taifa.


Amesema hayo Septemba 14, 2023 wakati akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Prof. Adelardus Kilangi alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma, kuzungumzia namna ya kunufaika na fursa za Sekta ya Madini zilizopo baina ya Mataifa hayo mawili.


Waziri Mavunde amesema kuwa mwelekeo wa Sekta ya Madini hadi kufikia mwaka 2030 ni kuongeza mchango wa sekta katika Pato la Taifa kwa kufungamanisha uchumi na sekta zingine zikiwemo za kilimo na viwanda.


“Kipaumbele chetu ni kuiwezesha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Tanzania (GST) lengo ni kufanya utafiti wa kina zaidi kwa kupiga picha za juu asilimia kubwa ya miamba tofauti na sasa ambapo ni asilimia 16 tu ya eneo lote. Upatikanaji wa taarifa hizi sio kwamba utasaidia Sekta ya Madini pekee, bali Sekta ya Kilimo kwa kujua miamba yenye maji pamoja na malighafi za viwanda kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea na bidhaa nyinginezo" amesema Mavunde.


Ameongeza kuwa ipo fursa kupata soko jipya la Madini ya vito nchini Brazil ili kuongeza wigo wa masoko mbali na nchi za Bara la Asia.
Kwa upande wake Balozi, Prof. Adelardus Kilangi anayeiwakilisha Tanzania nchini Brazil amempongeza Mhe. Mavunde kwa kuteuliwa na kuapishwa kuwa Waziri wa Madini na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuahidi kufanyia kazi suala la masoko ya madini ya vito nchini Brazil.


Amesema kuwa, zipo kampuni za Brazil zinazouza mashine za kuchonga na kung’arisha madini ya vito kwa ubora wa kimataifa kwa bei rahisi kwa ajili ya kuongeza thamani madini.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages