Breaking

Wednesday 4 October 2023

SEKTA YA MADINI KUFUNGAMANISHWA NA MIPANGO YA TAIFA UWEKEZAJI



Imeelezwa kuwa, Wizara ya Madini imeweka Mipango ya kuhakikisha Sekta Madini inafungamanishwa na mipango ya taifa ili kuwa na Matumizi yenye tija katika rasilimali za nchi hususan katika Sekta ya Madini.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 4, 2023 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde alipokutana na Waziri Ofisi ya Rais Uwekezaji na Mipango Prof. Kitila Mkumbo wakati wa kikao kifupi kilicholenga kujenga mahusiano mazuri ya uwekezaji nchini Ofisi za Wizara ya Madini Jijini Dodoma.

Amesema ushirikiano wa Wizara hizo mbili utaimarishwa ili Sekta ya Madini iweze kuingizwa katika mipango yenye tija kwa taifa na hatimaye kukuza uchumi wa madini.

Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa madini ni sayansi hivyo Sekta ya Madini itahakikisha inafanya utafiti wa madini nchini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kuvutia wawekezaji nchini.

"Lazima tupate taarifa sahihi za madini yaliyopo nchini hususan kwenye mahitaji makubwa ya madini muhimu na madini mkakati ili madini hayo tuyachimbe kwa kiasi kikubwa nchini," amesema Waziri Mavunde.

Kwa upande wake Prof. Kitila Mkumbo ,amesema Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji inaratibu na kuweka mazingira mazuri yanayoratibika kwa uwekezaji katika Taasisi za Umma

Ameongeza kuwa, kuhusu Madini Muhimu na Madini Mkakati Prof. Kitila amesisitiza mahitaji ya madini hayo duniani iwe chachu kwa Tanzania kutumia fursa hiyo katika kujenga mazingira bora ya kiuchumi ikiwa pamoja na kuibua maeneo mapya ya uwekezaji.

Pia, Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini Angelo Haule amesema mapendekezo ya Vipaumbele kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 ni kuendelea kufanya utafiti wa jiofizikia kwa kutumia ndege (High Resolution Airborne Geophysical Survey) na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji maduhuli na utoaji wa leseni.

"Tutaimarisha uwekezaji na Teknolojia katika Sekta ya Madini ili kuendeleza madini muhimu na madini mkakati katika kuhamasisha uwekezaji, biashara na uongezaji thamani Madini," amesisitiza Haule.


Vile vile, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba amesisitiza kuwa, kama Dira 2030 ya wizara Madini ni Maisha na Utajiri Sekta ya Madini itafanya utafiti ili kufikia maeneo mengi nchini na kuwawezesha wachimbaji wadogo kuchimba kwa tija badala ya kubahatisha.

Kikao kimehudhuriwa na Watendaji mbalimbali kutoka wizara hizo mbili na kwa pamoja wameahidi kushirikiana ili kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages