Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia mkoa wa kihuduma Kinyerezi imetoa rai kwa watumishi wake kuzingatia nidhamu na uwajibikaji wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Rasilimali watu DAWASA Kinyerezi, Ndugu Bakari Makilagi na kuwasisitiza kuwa uwajibikaji ni msingi wa ufanisi wa kazi na ndio unaoleta mafanikio ya kazi kwenye utendaji.
Ameongeza kuwa nidhamu mahala pa kazi ni msingi wa huduma bora hivyo ni vyema kila mtumishi aweke nidhamu kama kipaumbele ili kuhakikisha huduma zinazotolewa na DAWASA zinawafikia kwa ubora wateja.
"Watumishi wanabeba taswira ya Mamlaka kwa wateja, hivyo niwasihi kuwajibika ili kuleta matokeo chanya kwa mamlaka lakini pia jamii, kila mtumishi atakapoweka nidhamu mbele ndivyo ufanisi utakavyoongezeka."ameeleza
Ndugu Makilagi amesema DAWASA kupitia kitengo Cha Rasilimali watu na kitengo Cha mawasiliano hutumia njia mbalimbali kutoa miongozo ya utumishi wa umma kwa watumishi, kujenga na kuongeza uwezo ili kuongeza ufanisi mahala pa kazi.
Mkoa wa kihuduma Kinyerezi unahudimia takribani wakazi 16000 katika kata za Kinyerezi,Ukonga, Gongo la Mboto, Kipawa,Kwembe, Bonyokwa, Pugu station, Saranga na Msigani.