Breaking

Tuesday 7 May 2024

MJADALA WA KISERA WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KUENDELEZA UWEKEZAJI FEDHA KWENYE HEWA YA UKAA NCHINI TANZANIA

Dar es Salaam, 7 Mei 2024: Programu ya CookFund inayotekelezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Maendeleo ya mitaji (UNCDF) chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) wameandaa mdahalo wa kisera wenye kauli mbiu “Nishati safi ya kupikia na uwekezaji fedha kwenye hewa ya ukaa’ jijini Dar es Salaam.

Mjadala huu umelenga kujadili njia za kutengeneza mazingira wezeshi kwa ajili ya makampuni na mashirika ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye mnyororo wa thamani wa nishati safi ya kupikia kwenye biashara ya hewa ya ukaa. Mjadala huo ni mwanzo wa mfulululizo wa mijadala inayolenga kutatua changamoto za kisera zinazokwamisha matumizi endelevu ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania.

Mjadala huo ulihudhuriwa na wadau muhimu kutoka serikalini na sekta binafsi wakiwemo: Kamishna msaidizi wa nishati mbadala na umeme kutoka wizara ya nishati Mhandisi Styden Rwebangira na Seleboni Mushi, ofisa misitu kutoka wizara ya maliasili na utalii. Wachokoza mada walikuwa ni: Tajieli Urio kutoka SouthPole, Jaqueline Ngullo kutoka UpEnergy; Dr. Paul Lyimo, afisa wa uhufadhumi kutoka kituo cha kitaifa cha kuratibu biashara ya kaboni (NCMC), na Lois Kassana, mwakilishi kutoka taasisi ya sekta binafsi tanzania (TPSF).

Mhandisi Rwebangira alieleza juu ya hatua zilizochukuliwa kuendeleza biashara ya hewa ya ukaa.
“Wadau wengi hawana ujuzi wa kitaalamu wa kutosha, jambo linaloonyehsa umihimu wa kujengewa uwezo. Ninafuraha kuona ushirikiano kati ya wizara ya fedha na mradi wa CookFund kupitia UNCDF na EU katika kuratibu maeneo ya majaribio ya hewa ya ukaa kwa lengo la kutatua changamoto kupitia uidhinishwaji na uthibitishwaji.”

Kwa upande wake, Lois Kassana, mchambuzi wa sera kutoka TPSF aliainisha kuwa mipango ya biashara inatakiwa iwe na uwezo wa kukopesheka na kutoka kwa mabenki, iwe na utaalam, na uhalisi wa kibiashara unaohitajika kwa ajili ya kutengeneza fursa za masoko.

Mjadala huu ulihusisha utambuzi wa mapendekezo ya maboresha kama vile kurahisisha maombi na usajili na kuongeza ushirikiano baina ya wadau. Mkutano huo uliweka jukwaa la kubadilishana taarifa kuhusu fursa zilizopo za kuwekeza fedha kwa ajili ya sekta za umma na binafsi.

Meneja Programu na Mtaalamu mwandamizi wa Fedha kutoka UNCDF, Imanuel Muro, alisema kuwa jukwaa la maliasili ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza mjadala wa uwekezaji fedha endelevu ambao unahitajika zaidi ili kuanzisha hatua madhubuti za biashara ya hewa ya ukaa kwenye nishati safi ya kupikia nchini Tanzania.

Imanuel Muro, (kulia) Meneja wa mradi wa CookFund na Mtaalam Mwandamizi wa Fedha kutoka shirika la mfuko wa maendeleo ya mitaji la umoja wa mataifa (UNCDF) akizungumza wakati wa Mjadala wa kisera wa nishati safi ya kupikia na kuendeleza uwekezaji fedha kwenye hewa ya ukaa nchini Tanzania.

Jacqueline Ngulla (wa pili kulia), Meneja wa Operesheni kutoka UpEnergy akizungumza wakati wa mjadala wa kisera wa nishati safi ya kupikia kuendeleza uwekezaji fedha kwenye hewa ya ukaa nchini Tanzania. Kulia ni Tajiel Urioh, Mshauri mwandamizi wa sera ya hali ya hewa, fedha, na masoko ya hewa ya ukaa kutoka South Pole; Dkt Paulo Lyimo, Mtafiti na Afisa bio anuai kutoka kituo cha kitaifa cha kuratibu biashara ya kaboni (NCMC) na Lois Kassana (wa kwanza kushoto) mchambuzi wa sera kutoka Taasisi ya Sekta binafsi Tanzania (TPSF).
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages