Breaking

Saturday 11 May 2024

MWENGE WA UHURU WARIDHIKA HUDUMA YA MAJI KIGAMBONI

 


Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndugu Godfrey Mnzava ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kuboresha huduma ya majisafi katika Wilaya ya Kigamboni kupitia mradi wa uendelezaji wa visima virefu.

Ndugu Mnzava amesema hayo wakati wa ziara ya Mwenge wa uhuru kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo mradi wa uendelezaji visima virefu vya DAWASA na pia kupokea taarifa ya uzalishaji na usambazaji maji kupitia mradi huo. 

Mwenge wa Uhuru pia umeshiriki shughuli ya upandaji miti rafiki ya mazingira kuzunguka eneo la visima hivyo.

Ndugu Mnzava amesema kuwa DAWASA imepiga hatua kwenye uzalishaji na usambazaji maji katika Wilaya ya Kigamboni kupitia mradi huo unaozalisha lita milioni 70 kwa siku.

"Lengo kuu la Serikali yetu ni kuhakikisha tunafikisha maji katika maeneo mengi zaidi na kupunguza umbali wa Mwananchi kwenda kutafuta huduma ya maji. DAWASA kupitia mradi huu imeongeza upatikanaji wa Maji kwa wananchi takribani 7500 wa hapa wilaya ya Kigamboni," ameeleza. 

Ndugu Mzanva amesema kuwa Mwenge wa uhuru kitaifa umeridhika na hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi na kupongeza jitihada za upandaji miti takribani 1800 katika chanzo cha maji. 

Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi Mhandisi Thadei Mwanjombe amesema kuwa katika jitihada za kuboresha huduma kwa wananchi wa Kigamboni, DAWASA imefanya maunganisho mapya kwa wateja 6,300 na kufanya idadi ya wateja wanaonufaika na mradi wa Maji Kigamboni kufikia 7,500 tangu mradi ulipozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2022. 

"Kisima hiki kimojawapo cha mfano tulipo hapa kina uwezo wa kuzalisha lita 300,000 kwa siku ambazo hupelekwa katika kisima cha kusukuma maji na kisha kupelekwa katika tenki ambalo husambazwa kwa Wananchi wa Wilaya za Kigamboni, Temeke na Ilala," amesema. 

Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa zimeongozwa na kauli mbiu kutunza mazingira na shiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ujenzi wa taifa endelevu. 

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages