Breaking

Thursday 29 August 2024

WANAHARAKATI WAPAZA SAUTI USHIRIKI WA WANAWAKE KWENYE UCHAGUZI, MASUALA YA JINSIA KATIKA DIRA YA TAIFA 2050


 Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP , Bi. Lilian Liundi akizungumza wakati wa kufunga Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 lililofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma kuanzia Agosti 27-29 , 2024
 Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP , Bi. Lilian Liundi akizungumza wakati wa kufunga Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 lililofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma kuanzia Agosti 27-29 , 2024 - Picha na Malunde Media


 

YATOKANAYO NA TAMASHA LA 7 LA JINSIA NGAZI YA WILAYA

TAREHE 27 –29 AGOSTI, 2024- WILAYA YA KONDOA, DODOMA

Kauli mbiu: “Dira Jumuishi ya 2050: Miaka 30 Baada ya Beijing Tujipange

Kuanzia tarehe 27-29 mwezi wa Agost 2024, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na mashirika yanayotetea haki za wanawake na usawa wa jinsia nchini, Vituo vya Taarifa na Maarifa, na washiriki wa semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS), kwa ufadhili wa wadau mbalimbali wa maendeleo, umefanya Tamasha la 7 la Jinsia ngazi ya Wilaya katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma.

Tamasha hili limeongozwa na mada kuu isemayo, “Dira Jumuishi ya 2050: Miaka 30 Baada ya Beijing Tujipange”, huku mada ndogo ndogo zikiangazia Miaka 30 ya Beijing: wako wapi wanawake viongozi; Rasilimali za taifa ziwanufaishe wananchi wa pembezoni; Harakati za kijamii na ushiriki wa makundi rika; Teknolojia, mabadiliko tabia nchi, masuala ya ukatili wa kijinsia;  na masuala ya kazi zenye ujira  na staha  kwa wanawake na vijana.

Tamasha hili limekutanisha zaidi ya washiriki 300 wanaojumuisha wananchi wa Kondoa, wanakituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Haubi, wawakilishi kutoka serikalini ngazi ya mkoa, wilaya na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, wadau wa maendeleo, AZAKI, vikundi vya kijamii, vikiwemo vituo vya taarifa na maarifa kutoka Mtwara Vijijni, Kondoa Vijijini, Kishapu, Lindi, Same, Mwanga, Babati, Morogoro Vijijini, Gairo, Kinondoni, Ilala, na Ubungo,  na wanaharakati ambao wamekuwa bega kwa bega na TGNP katika kuchagiza usawa wa jinsia.

Tamasha lilifunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule. Katika neno la ufunguzi alitambua mchango wa TGNP katika kuendeleza harakati za usawa wa jinsia tangu mwaka 1993 katika ngazi zote za kitaifa hadi katika ngazi za kijamii (kata) ili kuhakisha walengwa wanaohitaji elimu hii waipate, akitolea mfano kata ya Haubi ambayo alisema ni moja ya kata zinazohitaji sana elimu hiyo ya usawa wa kijinsia.

Aidha, alihamasisha wanakondoa kutumia fursa adhimu ya tamasha kutoa maoni yao kupitia eneo maalumu kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi kwa ajili ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050. Aliwataka pia wananchi kupenda kuhudhuria mikutano ya serikali ili kuweza kutambua fursa mbalimbali zilizopo serikalini na kuweza kunufaika nazo, akitolea mfano wa uwepo asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayotengwa kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, pamoja na uwepo wa dirisha la asilimia 30 ya zabuni za serikali kwa ajili ya kupewa makundi maalumu ikiwemo wazabuni wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Hii ni kwa mujibu wa sheria ya mamlaka ya usimamizi wa ununuzi wa umma (PPRA) sura namba 410 ya mwaka 2023 kifungu cha 64 kinachotaka Halmashauri na ofisi zote za serikali kutenga bajeti ya ununuzi kila mwaka kwa ajili ya wazabuni wanawake, vijana na makundi maalumu. Katika hotuba yake pia alifafanua dhamira ya serikali kugharamia matibabu ya wanawake wajawazito ambao wanawajibika kuleta nguvu kazi ya taifa na kusisitiza kuwa mtumishi yeyote anayekiuka maagizo hayo ni muhimu wananchi watoe taarifa kwa mamlaka husika na aliweza kutoa namba ambazo zinaweza kutumika kutolea taarifa za ukiukwaji wa maagizo hayo ya serikali kwa taasisi na watendaji wa vituo vya umma vya huduma za afya. 

Mgeni Rasmi pia aliweza kutoa Tuzo ya Heshima ya Marehemu Mama Mercelina Fwaja kwa familia yake kama sehemu ya kumuenzi, kusherekea na kutambua mchango wake katika kuanzisha harakati kondoa. na ambaye alitoa mchango mkubwa sana katika kuanzishwa na kuratibiwa kwa mitandao ya kijnsia ya kati (IGNs) hapa Kondoa, IGNs hizo zilitumika kuleta vuguvugu la ukombozi wa wanawake na usawa wa kijinsia katika wilaya mbalimbali nchini kwa kipindi hicho. Kutokana uzoefu, nguvu na ujasiri wake, Mercelina aliweza kuwakilisha wanawake wa mashinani katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) Addis Ababa, Ethiopia. Baadae, kwenda Washington, Marekani kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa, wakati Mheshimiwa Asharose Migiro akiwa uko kama balozi wa Tanzania.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Bi. Gemma Akilimali aliweza kudadavua kwa kina Mada kuu ya Tamasha hili.  Tamasha hili limetumika kama jukwaa la kutuwezesha kutafakuri kwa kina kuhusu utekelezaji wa Azimio na Mpangokazi wa Beijing, ambao unatimiza miaka 30. Baada tu ya Azimio la Beijing, nchini Tanzania kulikuwa na fursa ya kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, hivyo ilikuwa ni fursa nzuri sana ya kuingiza masuala ya kijinsia katika Dira hii. Na ukiangalia katika Dira hii, masuala ya Jinsia yaliweza kuingizwa kwa kiwango fulani.  Tunapotafakari miaka 30 ya Beijing, nchi yetu pia ipo katika mchakato wa kuandaa Dira 2050, hii ni fursa nyingine adhimu ya kuhakikisha kuwa Dira hii inaingiza kwa ufasaha masuala ya jinsia.  Mwaka huu pia, pamoja na mchakato wa kuandaa Dira, nchi yetu pia itakuwa na mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu 2024 na uchaguzi mkuu mwakani 2025, hivyo, wito wetu mkubwa ni ongezeko la ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi na uongozi.  Tamasha hili limetupa fursa ya pekee ya kutafakari maeneo haya matatu ya mada kuu ya tamasha ambayo yana mahusiano makubwa sana. Siku ya kwanza pia kulikuwa na jopo na majadiliano ya wazi lililojikita katika kutathmini miaka 30 ya Beijing, Tumetoka wapi, tuko wapi na tunaelekea wapi.

 

Katika siku ya pili ya Tamasha, washiriki walijikita kwenye tafakuri na mijadala kupitia warsha zilizoangazia maeneo muhimu matano(5) kama zilivyoainishwa katika mada ndogondogo za tamasha hapo juu. Warsha hizi zilitanguliwa na jopo na mjadala wa wazi uliojikita katika kutathmini Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na maandalizi ya Dira ya 2050. Jopo lilijadilia kwa kina masuala ya kijinsia yaliyoingizwa katika Dira ya 2025, na mapungufu ya jinsia. Jopo hilo lilijadili pia utekelezaji wa Dira ya 2025 ikilenga katika mafanikio, changamoto na masuala muhimu ya kijinsia  yanayotakiwa kuzingatiwa katika Dira ya 2050.

Yafuatayo ni baadhi ya mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa Dira 2025.

Uzingatiwaji wa masuala ya kijinsia katika sera za kisekta, sheria na program, ikiwemo Sera ya huduma za kijamii- Sera ya Maji (2002); ya Elimu na Mafunzo (2014); na ya Afya (2007). Sheria ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Sura ya 272; Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410; Sheria ya Fedha ya Serikali ya Mitaa, Sura ya 290;

Juhudi hizi zimesaidia katika ongezeko la upatikanaji wa maji kutoka asilimia 50 mwaka 2000 mpaka asilimia 86.7 kwa mwaka 2020 kwa upande wa mijini, wakati upande wa vijijini, imetoka asilimia 55 mwaka 2000 hadi asilimia 72.3 mwaka 2020. Hata hivyo, hali halisi inaonesha kuwa miundo mbinu imeongezeka ila upatikanaji wa maji safi na salama pale yanapohitajika hayapatikani- Bomba si maji; na upatikanaji wake kwa gharama nafuu au bure kabisa.  Tumeona ongezeko la idadi ya wafanyakazi wanawake katika wizara ya maji, hadi kufikia mwezi April 2024 wanawake walikuwa ni asilima 60 ya wafanyakazi wa wizara ya maji, ambao ni sawa na wafanyakazi 5663. Hata hivyo, changamoto ni kwamba ni asilimia 24 tu kati ya hao wanawake, ambao ni sawa na nafasi 201, wapo katika ngazi ya maamuzi. Idadi hii ni ndogo sana.

Kwa upande wa afya imesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi nchini kutoka vifo 578 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2004/05 hadi kufikia vifo 238 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022/23. Kwa vifo vya Watoto chini ya umri wa miaka 5 kutoka 43 kwa vizazi hai 1000 mwaka 2015/16 hadi vifo 36 kwa vizazi hai 1000 mwaka 2022/23. Hata hviyo, katika mijadala yetu tumeona kuwa wanawake wanaoleta nguvu kazi wanalazimika kugharamia huduma za kujifungua kinyume na ahadi ya serikali.

Elimu ya afya ya uzazi kwa makundi rika hususani kwa vijana wa rika balehe bado haijatosheleza, na  maeneo ya vijijini elimu hiyo bado haijafika. Kwa upande wa kondoa, tumepokea visa vya vitendo ukatili wa kijinsia kuwa bado vipo juu, ikiwemo ndoa za utotoni, ulawiti, ubakaji, ukeketaji na vipigo kwa wanawake kutokana na mila na desturi na misingi ya dini.  Kadhalika, tumeona kwamba sababu nyingine inayochangia matukio ya ukatili wa kijinsia ni ongezeko la mmomonyoko wa maadili kwenye jamii zetu zinazochangiwa na uwepo wa  ajira zisizo na staha kwa wanawake. Kwa hapa kondoa, kumekuwa na changamoto ya ulevi uliokithiri na matumizi ya bangi ambayo yanapelekea athari kubwa kwa watoto na vijana kwa baadhi ya maeneo.

Kwa upande wa masuala ya kiuchumi, tumeona uingizwaji wa masuala ya jinsia kwenye sera kama vile Sera ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (2003); ya Taifa ya Kilimo (2013), ya Taifa ya Mazingira (2021); na ya Taifa ya Huduma ndogo za Fedha (2017). Hatua hizi zimechangia kuwepo kwa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wanawake, vijana na makundi maalumu kama uwepo wa mikopo ya kilimo kupitia benki ya taifa ya kilimo pamoja na programu ya kesho iliyo bora (BBT); pamoja na mifuko mingine 19 ya uwezeshaji wananchi kiuchumi katika viwanda na biashara.

Hata hivyo, tumeona kwamba bado kuna upungufu au ukosefu wa upatikanaji wa taarifa hizi za fursa kwa wanakondoa, na wakati mwingine kumekuwa na taarifa zisizo sahihi au zinazochanganya. Hivyo, kuwa ni changamoto kwa makundi haya kunufaika na fursa hizi zilizopo. Licha ya kuwepo kwa fursa nyingi za kiuchumi, tumeona kwamba bado wanawake wanaendelea kuelemewa na mzigo mkubwa wa kazi zisizo na ujira inayopelekea kuwapunguzia muda wa kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali, ambazo zinaweza kuwaingizia kipato.

Kwa upande wa uwakilishi na ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi na uongozi, tumepiga hatua ambapo mihimili miwili ya dola inaongozwa na wanawake, mhimili wa serikali Mheshiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa kwanza mwanamke Tanzania, na kwa upande wa Bunge tuna Spika wa Bunge Mheshimiwa Dk. Tulia Ackson, ambaye ni mwanamke wa pili kuongoza muhimili huo wa Bunge baada ya Mheshimiwa Anna Semamba Makinda. Hata hivyo, ushiriki wa wanawake katika ngazi ya serikali ya mitaa wenyeviti wa vijiji wanawake ni asilimia 2.1 ya wenyeviti wote; na Wenyeviti wa vitongoji ni asilimia 6.7 ya wenyeviti wote wa vitongoji, kwa mujibu wa Ripoti ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ya mwaka 2019.

Kwa hapa kondoa tumeona bado kuna changamoto, wanawake hawashiriki vya kutosha katika michakato ya uibuaji wa fursa na vikwazo vya maendeleo na mikutano ya kusomewa mapato na matumizi katika ngazi ya vijiji/mitaa na kata, na wale wanaoshiriki hawachangii vya kutosha kutokana na mila na desturi na misingi ya dini kandamizi.

Suala la mabadiliko tabia nchi ni janga la kidunia, na Tanzania sio kisiwa. Bado uelewa ni mdogo juu ya tabia ya nchi, teknolojia na masuala ya jinsia, na uwekezaji wetu katika kuzuia na kukabiliana na athari za mabadiliko tabia nchi bado ni mdogo.  Kwenye  kilimo, tumeona kwamba bado kuna changamoto kubwa ya umiliki wa ardhi kwa wanawake, ambapo ni takribani asilimia 20 tu ya wanawake wanaomiliki ardhi. Pia, kuna changamoto katika kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao kutokana na ardhi kuwa zimechoka, mbegu zinazotumika katika uzalishaji ni za gharama kubwa na haziwezi kutumika zaidi ya mara moja. Pia, kuna upungufu wa taarifa zinazowasaidia wanawake wakulima kuyafikia masoko ya kimakakati kwa ajili ya mazao yao, ambao wanalazimika kuuza mazao yao yakiwa shambani na hivyo kuuza kwa gharama ambazo si za soko. Kwa baadhi ya maeneo ya kondoa kumekuwa na ucheleweshwaji wa pembejeo za kilimo hususani Mbegu na Mbolea.  

Kutokana na changamoto hizo, washiriki wa tamasha hili wametoka na mapendekezo yafuatayo:

Kwa serikali:

1.     Iongeze bajeti kuboresha huduma za jamii ili ziweze kuwafikia wananchi, hususani waliopembezoni kwa urahisi na gharama nafuu au bure.  Kwa mfano; kuwaongezea mamlaka za maji bajeti za kuhakikisha kuwa maji yanasambazwa na yanapatikana wakati wote katika miundo mbinu iliyopo, hasa maeneo ya vijiji vya ndani ndani.  Bajeti ya maji bado haijapewa kipaumbele ni haizidi asilimia moja ya bajeti kuu.

Pia, tunapenda kuona kwamba wilaya na halmashauri  zinatengewa fedha za kutosha za kutekeleza afua za kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa kundi rika balehe. Kuongeza uwekezaji wa kibajeti ili kuondoa kabisa vifo, vinavyozuilika, vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga na wale walio chini ya miaka mitano, gharama hizi za uzazi zinapaswa kutolewa bure kabisa. Bima ya afya, ambayo ni rahisi kupatikana na yenye gharama nafuu na inayoweza kulipia huduma bora za afya kwa kila mwananchi.

Kwa upande wa elimu ni uwekezaji katika kuweka mazingira bora ya elimu hususani kwa makundi maalumu ili wawaweze kupata elimu bila shida, kwa mfano mabweni kwa Watoto wanaoishi mbali na shule, miundo mbinu rafiki kwa Watoto wanaoishi na ulemavu, upatikanaji wa miundo mbinu na huduma rafiki kwa Watoto wa kike wakiwa katika hedhi; pia kuweka mazingira wezeshi kwa wasichana wanaorudi shuleni na Watoto wao baada ya kupata kujifungua.

Aidha, tunapenda serikali itenge bajeti kuwawezesha maafisa katika ngazi ya kata na vijiji kufikia vijiji mbalimbali kuwajengea wananchi, hususani wanawake uwezo na kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili na kuwapa taarifa za fursa zilizopo na namna wanaweza kuzitumia ili kunufaika nazo. Mfano Maafisa Maendeleo ya jamii, Ustawi wa jamii, Ugani n.k

2.     Tunatoa wito kwa wadau mbalimbali kusaidia wanawake kuingia katika nafasi za maamuzi na uongozi katika ngazi zote, kuanzia vitongoji, vijiji/mitaa, kata, wilaya hadi taifa ili kuongeza idadi ya wanawake katika ngazi za maamuzi na uongozi. Tunatarajia Wilaya hii ya Kondoa itakuwa ya mfano katika kuhakikisha kuwa wanawake wanaongezeka hadi kufikia 50/50 katika nafasi za mamuzi katika ngazi na sekta zote.

3.     Serikali ya mkoa wa Dodoma iimarishe usimamizi wa utekelezaji wa agizo la serikali la matibabu bure kwa wanawake wanaojifungua kwa kutoa hizo namba na namna ya kutoa taarifa za ukiukwaji kwenye zahanati, vituo vya afya, hospoitali, na serkali za vijiji.

4.     Tunashauri halmashauri zitengeneze mwongozo wa maadili wa uendeshaji na usimamizi wa shughuli za baa, klabu n.k ili kuepuka kuendeleza vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na wasichana vinavyofanyika katika maeneo hayo.

5.     Tunashauri serikali ishirikiane na wadau kuhakikisha kuwa wakulima wanapata elimu ya mabadiliko tabia nchi na teknolojia mbalimbali zinazosaidia katika kuzuia na kukabiliana na mabadiliko tabia nchi, ikiwemo kubainisha, kushirikisha, kujifunza na kutumia mbinu bunifu za wakulima wnaotumia kukabiliana na athari za mabadiliko tabia nchi na kuziendeleza.  Kwa mfano kwa upande wa kondoa, kutokana na ardhi kuwa imechoka, na ikiwekwa mbolea inahamishwa wakati wa mvua, wameanza kutumia teknolojia ya mbegu 9 na jembe la kondoa; na upande wa mamire, wamekuwa wakitumia kilimo ikolojia. 

Kwa wananchi.

i.               Tunatoa wito kwa wananchi kushiriki katika mchakato wa bajeti kuanzia mchakato wa kuibua fursa na vikwazo vya maendeleo, kuweka vipaumbele, kutenga, kutekeleza na kufanya tathmini ya utekelezaji wa hiyo bajeti kwa mlengo wa jinsia.

ii.             Tunatoa wito kwa AZAKI na wadau wengine kutufatilia na kufanya uchambuzi wa utekelezaji wa masuala ya jinsia yaliyoingizwa kwenye sera, sheria, mipango na bajeti na kutoa taarifa za utekelezaji zinazoonesha changamoto na mapendekezo ya namna ya kutatua hizo changamoto.

iii.            Wananchi wafuatilie utolewaji wa huduma za afya za mama na mtoto bure, na kutoa taarifa pale ambapo agizo hilo halitekelezwi.

iv.            Tunapoelekea chaguzi za serikali za mitaa na uchguzi mkuu, AZAKI, vikundi, vituo vya taarifa na maarifa, wanajamii na vyombo vya Habari kwa pamoja, washirikiane kutoa elimu kuhusu madhara ya  ukatili wa kijinsia ikiwemo rushwa ya ngono wakati wa  uchaguzi; pia, kuhamasisha jamii kutoa taarifa pindi wanapobainisha vitendo hivyo.

v.              AZAKI, vikundi, vituo vya taarifa na maarifa, wanajamii na vyombo vya Habari kuendelea kutoa elimu  na kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa wanawake kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu kama wapiga kura, watia nia na wagombea. Hii itasaidia kuongeza ushiriki wa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu katika vikao vya kimaamuzi kuanzia katika ngazi ya Kijiji, na kata; na kupaza sauti za madai yenye tija kwa makundi maalumu.

vi.            Tunahamasisha wananchi kuchukua hatua ya kutafuta taarifa za fursa mbalimbali zilizopo katika ngazi mbalimbali.

vii.          Tunatoa wito kwa jamii kuimarisha suala la malezi katika ngazi ya familia yanayoelekeza katika kuleta usawa wa jinsia, maadili katika jamii pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana katika nyanja zote.

viii.         Kujenga nguvu za pamoja katika kuhakikisha kuendeleza usawa wa jinsia, katika nyanja zote- kiuchumi, kisiasa na kijamii katika maeneo yao

Katika siku ya tatu ya Tamasha washiriki walifanya majumuisho na kuweka mikakati  ya namna ya kutekeleza mapendekezo yaliyotokana na warsha. Tamasha lilihitimishwa kwa kuwasomea washiriki mapendekezo yaliyotokana na warsha na mikakati ya namna ya kutekeleza mapendekezo hayo.

Tunatoa shukurani kwa wadau wa maendeleoa wakiwemo Ubalozi wa Uswidi, CrossRoads International, UN Women, Chuo cha kimataifa cha Coady- Canada, Ubalozi wa Ireland, Ubalozi wa Canada kupitia Seedchange na Aga Khan Foundation kwa kuliwezesha kirasilimali tamasha hili kufana; na mashirika wenza wakiwemo CAMFED, WAJIBU, Chuo cha Serikali za Mitaa- Hombolo, Policy Forum, PELUM Tanzania, WFT na Msichana Initiative kwa ushiriki wao katika maandalizi ya tamasha, kushiriki na kuwezesha katika warsha mbalimbali zilizojadiliwa kwenye tamasha.

Taarifa hii imeandaliwa na:

Idara ya Habari,

Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP


 Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP , Bi. Lilian Liundi akizungumza wakati wa kufunga Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 lililofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma kuanzia Agosti 27-29 , 2024- Picha na Malunde Media
 Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP , Bi. Lilian Liundi akizungumza wakati wa kufunga Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 lililofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma kuanzia Agosti 27-29 , 2024
 Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP , Bi. Lilian Liundi akizungumza wakati wa kufunga Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 lililofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma kuanzia Agosti 27-29 , 2024
 Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP , Bi. Lilian Liundi akizungumza wakati wa kufunga Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 lililofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma kuanzia Agosti 27-29 , 2024 
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Gemma Akilimali akizungumza wakati wa kufunga Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 lililofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma kuanzia Agosti 27-29 , 2024 
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Gemma Akilimali akizungumza wakati wa kufunga Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 lililofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma kuanzia Agosti 27-29 , 2024 
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Gemma Akilimali akizungumza wakati wa kufunga Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 lililofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma kuanzia Agosti 27-29 , 2024 
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Gemma Akilimali akizungumza wakati wa kufunga Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 lililofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma kuanzia Agosti 27-29 , 2024 
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Gemma Akilimali akizungumza wakati wa kufunga Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 lililofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma kuanzia Agosti 27-29 , 2024 


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages