Breaking

Thursday 26 September 2024

TBS YATOA MAFUNZO KWA WAKULIMA KUKABILIANA NA SUMUKUVU KILOSA

SHIRIKA la viwango Tanzania (TBS) limetoa mafunzo kwa wakulima wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro jinsi ya kukabiliana na sumukuvu kwenye mazao ya mahindi na karanga kwa lengo la kupata chakula salama na kulinda masoko ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Septemba 26,2024, Kilosa mkoani Morogoro, Afisa udhibiti mwandamizi (TBS) Gerald Magola amesema wameamua kufanya zoezi hilo la kutoa elimu ili kuhakikisha watu wanakula chakula salama kwani wamebaini sumu hiyo hatarishi inapatikana kwa wingi kwenye mazao ya mahindi na karanga.

Amesema wanatarajia mazao yatakayotoka katika maeneo waliyotoa elimu ya kukabiliana na sumukuvu yatakuwa ni salama kwa matumizi ya binaadamu kwani yatakuwa na tahadhari zote za kudhibiti kuingia kwa sumu hiyo.

Kwa upande wake Afisa Udhibiti Ubora TBS, Kilango Kaiza amesema kuondokana na changamoto ya sumukuvu inawezekana kwa kufuata kanuni bora za kilimo kuanzia hatua ya maandalizi ya shamba,upandaji,uvunaji na hata katika hatua ya usafirishaji.

"Wakulima wanahimizwa kuzingatia kanuni bora za kilimo,wanapokuwa wanandaa mashamba yao kwa wakati,wanapopanda mbengu bora na kupanda kwa nafasi, wanapopalilia kwa wakati pamoja na kutumia mbolea, hata wanapoanika mazao yao wanashauriwa kuanika kwenye vichanja au maturubai". Amesema

Pamoja na hayo Kaiza ameshauri kuwa katika zoezi la usafirishaji wa mazao tahadhari zote zinatakiwa kuchukuliwa ili kuhakikisha mazao hayapati unyevunyevu au kunyeshewa na mvua.

Nae Mkazi wa kata Msololo wilayani Kilosa, Abdallah Issa ameishukuru TBS kuwapatia mafunzo hayo kwani mpaka sasa wakulima wa eneo hilo wanahifadhi mazao yao kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.

Vilevile Mkazi wa kata ya Ludewa, Betina Makawe amebainisha kuwa TBS imewapatia uelewa wa kuitambua sumukuvu ambapo kwa sasa wanao uwezo wa kukabiliana nayo kwa kufuata taratibu bora kuanzia maandalizi,uhifadhi mpaka hatua ya mwisho mazao yanapomfikia mlaji.

Mafunzo hayo ya kukabiliana na sumukuvu yamefanyika katika kata 15 hadi sasa katika Mkoa wa Simiyu, Morogoro pamoja na Mkoa wa Tabora.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages