Breaking

Friday, 25 October 2024

TGNP, AKF WATAMBULISHA MRADI WA TUINUKE PAMOJA KUTATUA CHANGAMOTO KWENYE JAMII



Na Dotto Kwilasa, Malunde Blog-DODOMA

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Aga Khan Foundation (AKF) wamekutana Jijini Dodoma na wadau wa ngazi ya Taifa na Mkoa katika kikao cha mashirikiano juu ya mradi wa Tuinuke pamoja wenye lengo la kutatua changamoto za kijinsia zilizopo kwenye jamii.

Meneja mradi huo Nestory Mhando ameeleza kuwa jumla ya kiasi cha Shilingi bilioni nane za kitanzania zinatarajiwa kutumika kuteleza mradi huo wa Tuinuke Pamoja utakaosaidia uongeza chachu ya elewa kwa jamii kuhusu kutatua changamoto za kijinsia ndani ya kipindi cha miaka mitatu katika mkoa wa Dodoma.

Akizungumza  Oktoba 24,2024 Jijini Dodoma kwenye kikao cha mashauriano na wadau Mhando amesema fedha za ufadhili wa mradi huo wenye lengo la kuleta usawa wa kijinsia katika ngazi ya jamii zimefadhiliwa na Ubalozi wa Ireland ambapo utekelezaji wake unafanywa na mashirika mawili ambayo ni Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) pamoja na Aga Khan Foundation (AKF).

 "Utekelezaji wa mradi huu utahusisha kupeka rasirimali fedha kwa vikundi ambavyo vipo katika ngazi ya jamii vilivyo jikitaka kupambana na changamoto za usawa wa kijinsia,lengo la mradi ni kuhakikisha usawa wa kijinsia unachukua nafasi kubwa kwenye jamii, " ameeleza Meneja huyo
Ametaja malengo mengine ya mradi huo kuwa ni pamoja na kuinua wanawake na kufafanua kuwa kwenye eneo hilo kuna maeneo makuu matatu ikiwemo kupeleka rasilimali fedha kwa vikundi, eneo la pili ni kuwajengea uwezo vikundi ili viweze kuwa na taaluma stahiki kwenye utelezaji wa miradi ambayo watakuwa wamebuni.

Eneo jingine ni kuviunganisha vikundi vya wanawake pamoja na mitandao inayohusiana na masuala ya jinsia ,haki za wanawake na watoto, makundi maalumu na jamii kwa ujumla.

"Yote haya yanafanyika ili mashirika haya makubwa yaweze kujifunza lakini pia vikundi viweze kujifunza kutoka kwa mashirika hayo makubwa ,kwa lugha nyingine tunaweza kusema tunabadilishana uzoefu,halafu sasa ule uzoefu kwa pamoja uweze kutusaidia kuondoa changamoto za kijinsia katika jamii yetu na hatimaye kuwa na Jamii salama,"amefafanua Mhando

Mbali na hayo ameeleza kuwa Mradi huo pia utajikita kwenye eneo lingine la kuhakikisha kunakuwa na majukwaa ya mijadala ambayo yatawaleta pamoja Wadau wa maendeleo na Serikali ikiwa ni pamoja na wanaharakati ,vikundi mbalimbali na wanajamii.

"Majukwaa haya yatasaidia kuangalia muktadha mzima wa masuala ya kijinsia, changamoto za kijinsia na mikakati ya utekelezaji lakini pia namna ambavyo sasa tunaingiza masuala ya kisera kwenye mambo ambayo yanahitaji utatuzi wa kisera zaidi”,amesisitiza
Kwa upande wake Ofisa habari wa TGNP na mratibu wa mradi huo Monica John amesema mradi huo ni wa miaka mitatu na kwamba makubaliano ya utekelezaji ni kwa kipindi cha mwaka mmoja mmoja.

“Kwa huu mwaka wa kwanza kiasi ambacho tunaenda kukitumia ni takribani shilingi bilioni mbili ambazo katika hizo fedha asilimia 50 kitaenda moja kwa moja kwenye ile jamii tunayoilenga, hii inamaaisha vikundi ambavyo vimejikita kwenye masuala ya kijinsia kwasababu ndicho tunachokitaka na tunataka rasirimali nyingi iende huko,”amesema

John amesema katika mwaka wa pili na wa tatu wanatarajia kuwa na kiasi kingine ambacho kitakamilisha kiasi hicho cha bilioni nane ambazo zimewekezwa ili kuwa na jamii yenye usawa.

“Malengo yetu ni kuona tunakuwa na Jamii inayoishi kwenye usawa ambayo haina vitendo vya ukatili dhidi ya jinsia au dhidi ya mtu yoyote lakini pia jamii ambayo inazingatia usawa, haki na wajibu pamoja na nafasi sawa katika nyanja zote za uongozi lakini pia katika umiliki wa rasilimali”,amefafanua

Aidha mratibu wa huyo amesema mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika hayo mawili ili kuwezesha vikundi katika ngazi ya jamii kuwa na harakati za pamoja za kuleta usawa wa kijinsia.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages