-Aipongeza Bodi ya Zabuni iliyomaliza muda wake kwa kazi nzuri iliyofanya
-Atoa tuzo kwa Wajumbe wa Bodi ya Zabuni iliyomaliza muda wake kutambua mchango wao
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy ameielekeza Bodi mpya ya Zabuni (Tender Board) ya Wakala kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu ili kuleta tija katika kazi zake.
Ametoa wito huo Mei 15, 2025 Jijini Dodoma wakati wa hafla fupi ya kuiaga Bodi ya Zabuni iliyomaliza muda wake baada ya kutumikia kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.
"Ninawapongeza walioteuliwa katika Bodi mpya ya Zabuni lakini niwasisitize mhakikishe mnatekeleza majukumu yenu kwa weledi ikiwemo kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Ununuzi wa Umma," alisisitiza Mhandisi Saidy.
Aidha, aliishukuru na kuipongeza Bodi ya Zabuni iliyomaliza muda wake kwa kazi nzuri iliyofanya kipindi chote cha muda wake.
Alisema Bodi ya Zabuni ni chombo na nyenzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi na aliwasihi walioteuliwa kuhakikisha wanatambua thamani waliyopewa.
"Bodi ya Zabuni ni muhimu sana katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Ununuzi za taasisi na ukiona umeteuliwa basi elewa kuwa wewe ni mtu sahihi na hakikisha hautoki nje ya taratibu," alisisitiza Mkurugenzi Saidy.
Vilevile alikipongeza Kitengo cha Ununuzi kwa kazi nzuri kinayofanya na aliwasisitiza kuielewa kwa undani Sheria ya Ununuzi ili kuwa na ununuzi wenye tija na uliyozingatia taratibu zote muhimu.
Aidha, akizungumza kwa niaba ya Bodi, Mwenyekiti wa Bodi iliyomaliza muda wake ambaye pia anaendelea kuhudumu katika Bodi mpya, Mhandisi Advera Mwijage alimshukuru Mkurugenzi Mkuu kwa sapoti aliyotoa muda wote alipohitajika pamoja na Kitengo cha Ununuzi ambao walifanya kazi kwa karibu na Bodi.
"Ninawashukuru Wajumbe wa Bodi waliomaliza muda wao, tumefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa kuhakikisha suala la Ununuzi kwa ujumla linafanyika kwa kuzingatia Sheria na miongozo iliyopo," alisema Mhandisi Advera.
Awali akizungumza wakati wa hafla hiyo, Katibu wa Bodi ya Zabuni REA ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi, Ndg. Mapesi Manyama alifafanua Sheria zinazoelekeza uundaji wa Bodi ya Zabuni kwa taasisi.