Breaking

Tuesday, 13 May 2025

WAZIRI MASAUNI AJIONEA KAMPUNI INAYOZALISHA UMEME KWA KUTUMIA TAKA



Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.Mha.Hamad M.Y Masauni ameongoza ujumbe wa Tanzania kutembelea kampuni ya Hafslund Celsion, kampuni inayojishughulisha na ukusanyaji na utengenishaji wa Taka katika Mainispaa ya Oslo nchini Norway.

Katika Ziara Hiyo Mhe Masauni aliambatana na Bi.Tone Tinnes, Balozi wa Norway nchini Tanzania pamoja na Maafisa kutoka Ubalozi wa Norway nchini Tanzania ambapo walipata fursa ya kujionea jinsi Kampuni hiyo inavyotumia mbinu mbalimbali za ukusanyaji wa Taka, inavyotenganisha Taka na kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwapo Umeme.

Akielezea jinsi taasisi hiyo inavyofanya kazi Mshauri wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Bw. Mads. A.Danielsen amesema kwamba Jiji la Oslo lina wakazi wapatao 725,000 ambapo kulingana na taarifa za mwaka 2023 kila mkazi huzalisha takribani kilo 157 za taka kwa Mwaka.

Bw. Danielsen amesema taasisi hiyo ina matawi matano ambayo yanajihusisha na upokeaji wa Taka zitokanazo na mimea, vigae,vyuma chakavu, fenicha zilizovunjika na magodoro taka hizi hujulikana kama Taka zenye ujazo mwingi ( Bulky Waste).


Taka zingine ni zile hatarishi, zitokanazo na vifaa vya Umeme na taka zinazoweza kurejelezwa kwa Matumizi Mengine.

Bw. Danielsen amesema ili kuhamasisha utenganishaji wa Taka Kampuni hiyo imekuwa ikitoa bure mifuko ya aina tatu ya kuhifadhia Taka, ambapo Mfuko wa Kijani umekuwa ukitumika kwa ajili ya taka za aina ya vyakula, Mfuko wa Zambarau taka za plastick na taka zinginezo huhifadhiwa katika mfuko wa Rangi Nyeupe.

Aidha, Ili kuhakikisha kuwa wananchi wa Jiji la Oslo wanatenganisha taka bila shurti, Bw. Danielsen amemweleza Mhe. Masauni na ujumbe wake kuwa wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kuelimisha Umma ikiwa ni pamoja na sinema, redio,magazeti, broshua, watu maarufu, mabango, matangazo kwenye vyombo vya usafiri, mitandao ya kijamii, muongozo wa kutenganisha taka, maonesho na shughuli mbalimbali za uhamasihaji.


Utenganishaji huo wa Taka umeiwezesha Kampuni ya Hafslund kuanzisha baadhi ya biashara kama uzalishaji maji yanayotokana na Mvuke unazalishwa baada ya kuunguza Taka, Biashara ya Umeme, Biashara ya Kaboni, uzalishaji wa Mbolea na uuzaji wa Vitu na vifaa vilivyotupwa ambavyo vinaweza kutumiwa na watu wengine.

Baada ya mkutano huo Ujumbe wa Tanzania ulipata fursa ya kutembelea kiwanda hicho na kujionea hatua mbalimbali za utenganishaji taka.

Kama nchi zingine duniani Tanzania nayo inazalisha taka ambapo utenganishaji wa taka hutoa fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzaliza bidhaa zingine zenye manufaa na kuzalisha ajira.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages