Breaking

Tuesday, 13 May 2025

TANZANIA YA 12 DUNIANI KWA ONGEZEKO LA WATALII



Na Samir Salum, lango la habari

Imeelezwa kuwa Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi ambazo zimevunja rekodi ya idadi ya juu ya watalii wa kimataifa huku ikishika nafasi ya 12 duniani kwa ongezeko la watalii.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana Mei 13, 2025, wakati wa Mkutano wa tatu wa majadiliano kati ya wadau wa utalii na Wizara ya Maliasili na Utalii uliofanyika Jijini Dodoma.

Waziri Chana ameeleza kuwa kwa mujibu wa Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) kupitia taarifa yake ya World Tourism Barometer ya Januari, 2024 imeitambua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi ambazo zimevunja rekodi ya idadi ya juu ya watalii wa kimataifa (Best performing destinations January to December, 2023).

“idadi ya watalii imeongezeka na kufikia 5,360,247 ambapo watalii wa ndani ni 3,218,352 na watalii wa nje 2,141,895 na mapato yatokanayo na shughuli za Utalii yapatayo Dola za Kimarekani Bilioni 3.3.”

“Kufuatia ongezeko hilo, Tanzania imetajwa na Shirika la Utalii Duniani (UN – Tourism) kuwa nchi ya kwanza Afrika kwa ongezeko kubwa la watalii wa kigeni ikilinganishwa na kabla ya UVIKO mwaka 2019, pia imeshika nafasi ya 12 duniani kati ya nchi bora zaidi kwa utalii " alisema Dkt. Chana

ameongeza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa katika Mkutano wa 13 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) mwaka 2022.

“Mkutano huu ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Utalii na maagizo ya Mheshimiwa Rais. Wizara yangu imejizatiti kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwenye sekta ya utalii ili kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa,”

“juhudi mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kukuza utalii, zikiwemo kuimarisha miundombinu, utoaji wa huduma bora na matumizi ya mbinu za kisasa za utangazaji kama vile filamu za Tanzania – The Royal Tour na Amazing Tanzania” alisema Waziri Chana.

Aidha waziri Chana amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza sekta ya utalii na kutoa wito wa kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha sekta hiyo inatoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi,Maliasili na Utalii Timotheo Mnzava amesema mkutano huo ni muhimu kwani inawakutanisha wadau wa sekta ya utalii na uhifadhi na kutoa nafasi ya kutoa mawazo na changamoto inayoikabili sekta hiyo na kuja na Suluhisho la changamoto hizo ili kuendelea kuiboresha.

“Sisi kama bunge tutajitahidi kuendelea kukutana na wadau ili yale mengine ambayo mtakuwa mmeshindwana serikalini au hamjaelewana serikalini au walikosa ujasiri wa kuyasema serikalini basi kwa sisi wawakilishi wao tutakuwa na ujasiri wa kuyasema na kuwasimamia ili mambo yaweze kwenda vizuri", amesema.

Kwa mwaka 2024 Tanzania imepokea tuzo kadhaa za kimataifa zikiwemo eneo linaloongoza Barani Afrika kwa Watalii (Africa’s Leading Destination), eneo linaloongoza kwa utalii wa Safari duniani (World’s Leading Safari Destination), 

Pia hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuendelea kuwa hifadhi bora duniani, na Mlima Kilimanjaro kuwa kivutio bora cha utalii Afrika (African Leading Tourism Attraction), huku Bodi ya Utalii Tanzania ikitajwa kuwa bodi bora ya utalii barani Afrika (Africa’s Leading Tourism Board).

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages