Breaking

Monday 28 February 2022

MTU MMOJA AUAWA, 10 WAJERUHIWA KATIKA MKUTANO WA CHAMA CHA UPINZANI - ZIMBABWE





Mtu mmoja ameuawa na wengine 10 kujeruhiwa katika mapigano kwenye mkutano wa chama cha upinzani huko Kwekwe, katikati mwa Zimbabwe.

Tukio hilo limetokea jana Jumapili Februari 27, 2022 ambapo Wafuasi wa Chama cha Wananchi (CCC) walivamiwa na kundi la watu waliokuwa na mikuki, mapanga, chuma na mawe.

Kwa mujibu wa Viongozi wa chama hicho wamesema kuwa Mtu mmoja aliuawa kwa kuchomwa kisu, wengine kuvunjika mifupa na majeraha mbalimbali.

Ghasia hizo zilimlazimu kiongozi wa chama Nelson Chamisa kuacha hotuba yake.

Chama hicho kiliwalaumu wafuasi wa Rais Emmerson Mnangagwa kuhusika na ghasia hizo, madai ambayo chama tawala kilikataa.

Haya yanajiri huku makundi ya kutetea haki za binadamu yakionya kuhusu kuongezeka kwa ghasia kabla ya uchaguzi muhimu mdogo uliopangwa kufanyika tarehe 26 Machi.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameonya kuhusu lugha za uchochezi katika kampeni hizo.

Mwishoni mwa juma makamu wa rais wa nchi hiyo alionya kwamba upinzani ungekandamizwa kama chawa, na hivyo kuzua hofu ya ghasia mpya.

Siku ya Jumamosi polisi walitumia vitoa machozi na maji ya kuwasha kutawanya mkutano mwingine wa CCC ambao ulikuwa umeidhinishwa na Mahakama Kuu.

Baadhi ya viti 28 vya ubunge na 122 vya udiwani vinawaniwa. Uchaguzi huo mdogo unaonekana kuwa mtihani kwa chama tawala cha Zanu-PF kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika 2023.

Kipindi cha kabla ya uchaguzi tayari kimekumbwa na madai ya hitilafu katika orodha ya wapigakura, ya upendeleo wa polisi na vyombo vya habari.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages