Breaking

Monday 28 February 2022

URUSI NA UKRAINE WAFANYA MAZUNGUMZO, RAIS ZELENSKY ALITAKA JESHI LA URUSI KUWEKA SILAHA CHINI




Televisheni ya taifa ya Russia imetangaza kuwa duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya wajumbe wa nchi hiyo na Ukraine imemalizika nchini Belarus.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Jumatatu Februari 28, 2022 yana lengo la kuzima moto wa vita vilivyoanza Alkhamisi iliyopita kati ya nchi hizo mbili.

Awali mkuu wa timu ya mazungumzo ya Russia huko Belarus alitangaza utayarifu wa Urusi wa kufikia makubaliano na Ukraine haraka iwezekanavyo.

Sambamba na jitihada zinazofanywa ya timu za mazungumzo ya Russia na Ukraine chini ya upatanishi wa Belarus ili kukomesha mzozo huo, moto wa vita bado unaendelea kufukuta na ripoti zinaonyesha kuwa mji wa Berdiansk umetekwa na jeshi la Russia.


Kabla ya mkutano huo kuanza, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliwataka wanajeshi wa Urusi kuweka chini silaha zao, na kutoa wito kwa EU kuipatia Ukraine uanachama wa umoja huo mara moja.

Wakati huo huo mashambulizi ya makombora yanayofanywa na jeshi la Ukraine na makundi ya kitaifa yenye msimamo mikali yanaendelea dhidi ya maeneo ya makazi ya raia huko Donbas, huku majeshi ya Russia yakichukua udhibiti wa mji wa kusini mashariki wa Berdyansk katika siku ya tano ya operesheni za kuilazimisha serikali ya Ukraine kusitisha mashambulizi dhidi ya wakazi wa Donbas.


Mkuu wa timu ya Russia katika mazungumzo hayo Vladimir Medinsky amesema leo Jumatatu kwamba "Ikiwa mzozo wa Ukraine utaendelea, idadi ya wahanga itaongezeka, kwa hivyo tunataka kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo, na bila shaka makubaliano haya yanapaswa kuwa na maslahi ya pande zote mbili."

Mapigano ya mitaani yanaendelea baina ya wanajeshi wa Ukraine na vikosi vya Russia katika mji mkuu Kyiv.

Mashambulizi ya jeshi Russia yalianza Alkhamisi iliyopita baada ya Rais Vladimir Putin wa Russia kutangaza kwamba jeshi la nchi hiyo limeanzisha "operesheni maalumu ya kijeshi" katika eneo la Donbass nchini Ukraine na kwamba lengo la operesheni hiyo ni kuiondoa Ukraine katika hali ya kijeshi na kwamba hana nia ya kuvamia ardhi ya nchi hiyo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages