Breaking

Tuesday 22 March 2022

BASATA, COSOTA TOKENI WASAIDIENI WASANII, HAKUNA MSANII MKUBWA KULIKO NCHI - WAZIRI MCHENGERWA




Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amezielekeza Taasisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Taasisi ya Hakimiliki nchini (COSOTA) kukamilisha zoezi la kuwasajili wasanii  wote    hususan  wale wa kubwa ambao  bado hawajasajiliwa  huku akisisitiza kuwa hakuna msanii  mkubwa  kuliko nchi.


 Waziri Mchengerwa ametumia muda wa takribani masaa matatu kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali hususan ya wasanii na kutoa maelekezo ya kusaidia wasanii wote nchini na kuwaunganisha ili waweze kufaidika na kazi zao alipokuwa mgeni rasmi kwenye kikao cha Baraza la wafanya kazi  la Wizara yake Machi 21, jijini Dodoma.


“Leo  nataka  niwaelekeze BASATA na COSOTA na sitaki  kurudia rudia jambo  hili.Hatutegemei  kusikia  eti wamesajiliwa wasanii wachache, au kusikia msanii  mkubwa  hajasajiliwa tutaanza kuhoji uwezo wa wewe tuliokupa  dhamana”. Amefafanua Mhe Mchengerwa 


Amewafunda Watendaji wa Wizara na Taasisi zake  kwa kuwataka kuwa wanyenyekevu  na kutoa  huduma  kwa weledi  na kuwasaidia  wasanii kwa kuwa kupitia kazi zao  wanatoa mchango mkubwa kwa nchi  na Serikali inafaidika   kwa  kodi wanayoipata.


“Jukumu letu ni kuwaunganisha  wasanii wote bila kujali anatoka kundi gani kwa kuwa  hakuna msanii  mkubwa  kuliko nchi, kwa hiyo sisi tuliopewa mamlaka  twende  tukawanyenyekee wasanii hawa, wanatoa  mchango mkubwa wa ajira, nchi yetu inanufaika  kupitia  kodi mbalimbali.Pia ni muhimu   tukumbuke kwamba Wizara yetu inawagusa  zaidi ya asilimia  80 ya wananchi wake”.Amesisitiza Mhe. Mchengerwa.


Amekemea tabia ya kujifungia maofisini  kuwasubiri  wasanii wawatafute  na badala yake amewataka watendaji watoke  na kuwafuata wasanii waliko ili wawasaidie. 


Aidha amewataka  kutoa elimu kwa wasanii  ya  mambo mbalimbali kama jinsi ya kujisajili na masuala  mengine yanayowahusu ili wafanye kazi zao kwa rah ana kunufaika nazo.


Kuhusu kuwashirikisha  wasanii kwenye ngazi mbalimbali za maamuzi Waziri Mchengerwa amewataka watendaji  kutoa mapendekezo ya wajumbe wa bodi mbalimbali za tasnia za  michezo na sanaa  kwa wanamichezo na wasanii ili waweze kushiriki kikamilifu katika kusimamia biashara zao, kutafuta masoko na kulinda na kupigania haki zao moja kwa moja .


 Akitolea mfano  ya  Wasanii wa Kenya akina Juakali   amesema  ndiyo wanaosimamia  na kulinda haki zao ndiyo maana hawakubali sanaa  ianguke  kwa kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wameanguka wao. 


Kwa upande mwingine  Waziri Mchengerwa amewaagiza  Wakuu wa Idara na Vitengo  chini ya Wizara yake  kusimamia kwa  dhati suala la maadili ambapo amewahimiza kutumia  muda wao wa kazi kuhudumia wananchi  kwa kujibu  hoja za wananchi na kutatua kero  zao kwa haraka na ufanisi.


Amewataka   watumishi kutoa huduma bora kwa wananchi huku wakiongeza bidi kazini, uadilifu, uwajibikaji pamoja na kuzingatia sheria ambayo ndiyo misingi ya  utendaji wa kazi wa Serikali ya Awamu ya Sita  chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages