Breaking

Wednesday, 16 March 2022

WAHITIMU JESHI LA UHIFADHI WATAKIWA KUZINGATIA VIAPO VYA UTII KWA SERIKALI KULINDA RASILIMALI MISITU

 


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amefunga mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi kwa askari wapya 43 ambao wanajiunga rasmi katika utumishi wa umma, hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza.


Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri Mary amewaasa wahitimu hao kutumia vyema ujuzi na weledi walioupata katika mafunzo hayo ili kulinda na kusimamia vyema rasilimali za misitu.


Amewataka kutunza siri za Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao na kuzingatia viapo vya utii kwa Serikali ili kuendelea kuyalinda maadili na maslahi ya Umma.



Aidha, amewakumbusha wahitimu hao kuwa na utu wanapotekeleza majukumu yao kwa kuepuka kutumia nguvu pale isipohitahika hasa wanapokutana na wahalifu katika mazingira yao ya kazi.

Awali, Naibu Waziri Mary amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa ajira kwa vijana hao.

“Kipekee nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali vijana na kutoa ajira katika sekta mbalimbali ikiwemo Sekta hii ya misitu ambapo leo vijana 43 wanapewa fursa ya kuitumikia nchi” amefafanua  Naibu Waziri Mary.



Mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi yamefanyika kwa watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yaliyolenga kuwanoa maafisa na askari kuingia rasmi katika mfumo wa Jeshi la Uhifadhi ili kusimamia vyema rasilimali za misitu na nyuki.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages