WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ametoa miezi mitatu kwa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), na Kampuni ya Kuhudumia Makontena Tanzania (TICTS), kuhakikisha wanashirikiana kumaliza msongamano wa meli zinazohitaji kushusha mzigo katika bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akikagua utendaji kazi wa TPA, Prof. Mbarawa ameagiza kuanzia sasa meli zinazoshusha mizigo zihudumiwe katika gati za TPA na TICTS ili kupunguza msongamano wa meli nyingi zinazosubiri kuingia bandarini.
"Kuanzia leo meli zishushe pande zote ili kuleta ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam sitaki kusikia kuna meli imekaa zaidi ya wiki mbili ikisubiri kuja kushusha mzigo hapa," amesisitiza Prof. Mbarawa.
Aidha ameiagiza TPA kufuatilia utendaji kazi wa TICTS ili kuona kama unaleta tija kwa bandari ya Dar es Salaam na kama hauleti tija kuchukua hatua za haraka ikiwemo kusitisha mkataba na kutafuta kampuni nyingine bandarini hapo.
Amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Bw. Erick Hamis kuhakikisha sehemu zilizo wazi zinaboreshwa ziwe za kisasa na kuongeza wigo wa kuhifadhi mizigo bandarini hapo.
"Hakikisheni mnaongeza maeneo ya kuhifadhia mizigo bandarini ili kupunguza msongamano na kitengo cha manunuzi cha TPA kiongeze kasi ya utendaji," amesema Prof. Mbarawa akiwa katika ziara hiyo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Erick Hamis amemhakikishia Prof. Mbarawa kuwa Maelekezo yake yatafanyiwa kazi kikamilifu na katika kipindi cha miezi mitatu kutoka sasa kutakuwa na mabadiliko makubwa ya kiutendaji bandarini hapo.
Upanuzi mkubwa uliofanywa katika bandari ya Dar es Salaam umeongeza idadi ya meli kubwa kutumia bandari ya Dar es Salaam hali inayochangia uwepo wa msongamano wa meli zinazosubiri kuingia katika bandari hiyo kushusha mizigo, hivyo utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mbarawa unaweza kuongeza tija na kuvutia meli nyingi zaidi kutumia bandari hiyo.