
Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Huduma za Tume, William Mtinya amesema kuwa Tume ya Madini imeandaa mikakati mbalimbali ya ukusanyaji wa madeni mbalimbali ya Serikali yatokanayo na ukusanyaji wa tozo ikiwemo kwenye shughuli za utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini ili kuendelea kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli linalowekwa na Serikali.
Mtinya amesema hayo kupitia mahojiano maalum kwenye kikao cha maafisa fedha kutoka Tume ya Madini Makao Makuu na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kinachoendelea jijini Dar es Salaam chenye lengo la kukusanya na kuandaa taarifa ya fedha kwa mwaka wa fedha 2021/2022 pamoja na kujiwekea mipango madhubuti ya kutekeleza kwa mwaka wa fedha 2022/2023, kubadilishana uzoefu na kujifunza mifumo mbalimbali ya malipo Serikalini.
"Wahasibu na maafisa fedha wanatakiwa kwa kushirikiana na maafisa madini wakazi wa mikoa kujenga mazingira mazuri ya ulipaji wa madeni kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kwa kukaa nao, kujadiliana nao na kuweka mikakati ya kulipa kwa awamu bila kuathiri shughuli zao za uzalishaji wa madini," amesema Mtinya
Kwa upande wake Meneja wa Fedha na Uhasibu wa Tume ya Madini Mwagule Dickson, akisisitiza juu ya ukusanyaji wa madeni, amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji na wafanyabiashara kuhusu Sheria ya Madini na kanuni zake, usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, ushirikishwaji wa watanzania kwenye Sekta ya Madini, (Local Content) na utoaji wa huduma kwa jamii zinazozunguka migodi ya madini (CSR) ambapo itawezesha kuwa na uchimbaji salama na endelevu hivyo kuwezesha sekta kuchangia kwa kiwango kikubwa katika uchumi wa nchi.
Wakati huohuo wakizungumza kwa nyakati tofauti maafisa fedha wamepongeza hatua ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba kuanza zoezi la uhamasishaji la ulipaji wa madeni kwenye Sekta ya madini na kusisitiza kuwa watakuwa mabalozi wazuri kwenye maeneo yao ya kazi kwenye kampeni ya uhamasishaji na kukusanya madeni.