Breaking

Tuesday 12 April 2022

"SERIKALI INANDELEA KUCHUKUA HATUA MBALIMBALI KULETA UNAFUU BEI YA MAFUTA" WAZIRI MAKAMBA




Na Mwandishi Wetu


Waziri wa Nishati January Makamba amesema serikali inahangaika usiku na mchana kuhakikisha inaleta unafuu wa bei za mafuta nchini huku akiwataka watanzania kuwa watulivu na kuepuka maneno ambayo yanaweza kuleta mfarakano.

Waziri Makamba amesema serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za muda mfupi na muda mrefu kwa lengo la kuleta unafuu kwa watanzania.

Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Watch Tanzania ukishirikisha kushirikisha watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) uliowashirikisha pia wadau mbalimbali wa mafuta Tanzania, waziri Makamba ameeleza baadhi ya hatua ambazo serikali imezichukua hadi sasa.

Waziri Makamba amesema serikali ina mpango wa kurahisisha kutoa mafuta katika meli kubwa zinazoingia nchini kwa kujenga mabomba marefu pamoja na kujenga hifadhi ya kimkakati ya mafuta.

“Tuna mpango wa kujenga mabomba marefu zaidi kwenda baharini, ili hata meli ikiwa umbali mrefu zaidi tuweze kushusha mafuta” ameeleza Makamba

Aidha amesema serikali sasa inajipanga kuwa na uwezo wa kuagiza mafuta kwa kutumia shirika la mafuta TPDC huku akisema hatua hiyo itasaidia kupatikana kwa wingi kwa nishati hiyo

“Tunataka sasa serikali iwe na uwezo wa kuagiza mafuta, hatuna maana ya kuiondoa sekta binafsi, uwezo huo ulipotea ila sasa tumeiagiza TPDC kuagiza na kushindana “

Katika hatua nyingine waziri huyo amesema kuwa serikali inaendelea kuzungumza na nchi rafiki kuona ni namna gani wanaweza kupata mafuta kwa bei nafuu hasa kwa kipindi hiki ambacho bei ya dunia imepanda

Katika mkutano huo Prof Godius Kahyarara ambaye ni Katibu mkuu wizara ya uwekezaji, viwanda na biashara amesema kuwa serikali haitawavumilia wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali ambao wanapandisha bei ya bidhaa kiholela bila kufuata utaratibu

“FCC tayari wamefanya tathmini na wamegundua baadhi ya maeneo ambayo bei zinachezewa tumewaagiza wachukue hatua, bei elekezi ziheshimiwe na hata bei zinapobadilika lazima wadau washirikishwe”- ameeleza Prof Godius Kahyarara
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages