Breaking

Wednesday 29 June 2022

WAKUU WA SHULE WAPEWA MAAGIZO MAZITO


Na Lango La Habari


WALIMU wakuu wa shule zote nchini wametakiwa kusimamia ipasavyo miradi yote inayotekelezwa na serikali katika shule zao ikiwemo kuhakikisha fedha zinazoletwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kutimiza azma ya serikali ya kuboresha sekta hiyo.

Aidha wameagizwa kusimamia vizuri nidhamu ya walimu na wanafunzi, kutoa motisha chanya kwa walimu na wanafunzi wao wanapofanya vizuri katika masomo yao na kuwa viungo vizuri kwenye jamii inayowazuguka.

Maagizo hayo yametolewa jana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Profesa Riziki Shemdoe alipokuwa akihitimisha semina ya utendaji kwa Wakuu wa shule za sekondari zenye kidato cha 5 na 6 na Maofisa Elimu wa Mikoa yote ya Tanzania Bara iliyofanyika Mjini Tabora.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Rais Samia, fedha nyingi zimeletwa katika shule mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za walimu, mabweni na ununuzi wa thamani.

Alibainisha kuwa haya yote yalilenga kuboresha miundombinu ya shule hizo ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ufundishwaji, kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuinua kiwango cha elimu.

‘Hakikisheni miradi yote inasimamiwa ipasavyo na fedha zinazoletwa zifanye kazi iliyokusudiwa, ninyi ndiyo mko karibu na watekelezaji miradi hiyo, msaidieni Mheshimiwa Rais, kinyume na hapo tusilaumiane’, alisema.

Profesa Shemdoe alisema zaidi ya shule 300 zimejengwa katika wilaya na majimbo yote ikiwemo kila kata ili kuhakikisha watoto wote wanaofaulu darasa la saba wanapata nafasi ya kujiunga kidato cha 1, hivyo akawataka kuzisimamia.

Alisisitiza kuwa kazi iliyoko mbele yao ni kusimamia sekta hiyo ili yale yote yanayofanyika yalete tija kubwa huku akibainisha kuwa jamii iliyoelimika na kupata ujuzi ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya taifa lolote.

Aliwataka kuhakikisha mazingira ya shule zao na miundombinu vinatunzwa vizuri ili viendelea kuwa bora huku akiwataka kuweka utaratibu mzuri wa kurekebisha miundombinu inapoharibika ili kutoathiri ufundishaji na ufundishwaji watoto.

Mwisho.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages