Breaking

Friday 22 July 2022

BILIONI 2.1 KUBORESHA KILIMO CHA PAMBA



Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI ya Tanzania imesaini mkataba wa zaidi ya Sh.bilioni 2.1 na nchi ya Brazili kwa ajili ya uboreshaji wa sekta ya kilimo bora cha zao la pamba nchini.

Utiaji saini mradi huo umewashirikisha Balozi wa Brazil nchini Tanzania Antonio Agustors Martin Cesar, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Brian Bogart na wadau wengine.

Mradi huo ulisainiwa Julai, 20 mwaka huu umelenga kuongeza thamani katika zao la pamba ujulikanao kama 'Beyond Cotton Project'

Mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 20 na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Bodi ya Pamba (TCB) pamoja na Wizara ya Kilimo.

Utiaji saini huo umefanyika kati ya Brazil (ABC ,UFCG ) Tanzania (TARI &TCB) na WFP(COE Brazil na WFP Tanzania.

Baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo Balozi Cesar, Kaimu Mkurugenzi WFP, Bogart, Gunga Mbavu ambaye alimwakilisha mgeni rasm ambaye ni katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo na Mkurugenzi TCB, Marco Mtunga wamesema kuwa kilimo bora cha pamba kitaimarisha uchumi wa Watanzania na wakulima kwa ujumla.

Kwa nyakati tofauti viongozi hao wameeleza kuwa mikataba ya uboreshaji wa kilimo cha pamba nchini kitaongeza ufaisi wa kipato cha wakulima wa zao hilo pamoja uchumi wa taifa kwa ujumla.

Balozi Cesar alisema Brazil wataendelea kushirikiana na nchi ya Tanzania kwa kuimarisha kilimo cha pamba nchini ili kuwa na tija katika zao hilo.

Alisema mradi wa kusaidia utafiti wa usalama chakula na lishe na kuongeza thamani ya zao la pamba utahusisha kaya 8,800 sawa na asiliia 50 vijana watakaonufaika.

Aidha ameeleza kuwa kwa mwaka 2030 kilimo kitakuwa kina uwezo wa kuzalisha asilimia 10 ya pato la taifa.

Naye Mkurugenzi TCB, Mtunga alisema pamba ni zao ambalo litaongeza tija kwa mkulima pamoja vijana kuweza kujikwamua kimaisha.

Katika hatua nyingine alisema mkataba wa kilimo bora cha pamba ni kuendeleza zao hilo na utafiti wa mbegu bora zisizoshambuliwa na wadudu na magonjwa kama ilivyokuwa hapo awali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk.Geofrey Mkamilo alisema taasisi hiyo itaendelea kufanya utafiti wa mbegu bora ambazo zitaongeza tija kwa wakulima wapamba.

Aidha, alisema mradi wa kilimo cha pamba utatekelezwa katika mkoa wa Mwanza katika Wilaya ya Magu, Misungwi na Kwimba.

Mwisho.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages