Breaking

Friday 22 July 2022

ZAIDI YA SH.MILLIONI 900 KUIPENDEZESHA TEMEKE



Na Mwandishi Wetu

ZAIDI ya zaidi ya Sh. milioni 998 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kuendeleza maeneo ya wazi na upandaji miti 1,927 katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, ili kufikia lengo la ‘Dar ya Kijani’.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) Manispaa Temeke, Mhandisi Paul Mhere wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo ambaye alikuwa anakagua ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Mwembeyanga.

Mhandisi Mhere alisema mradi huo wa Uboreshaji wa Viwanja vya Wazi (DOSU), Temeke itapanda miti 1,927, itaboresha Kiwanja cha Mpira Mwembeyanga, uwanja wa mpira wa kikapu, wavu, ngumi na sehemu ya kucheza watoto.

Meneja huyo anasema mradi huo utawezesha ujenzi wa eneo la Kumbukumbu ya Kudai Uhuru (Mwembeyanga Memorial), jengo la ofisi, vyoo vya umma, njia za watembea kwa miguu, maegesho na maeneo ya kufanyia biashara.

“Pia kutakuwa na sehemu za wazi kwa shughuli mbalimbali na kupandwa miti mipya 93 ili kutimiza dhana ya Dar es Salaam ya kijani,” alisema.

Alisema, baada ya kukamilika ujenzi wa maeneo hayo ya wazi yatakuwa chini ya Halmashauri lakini wananchi hawatatozwa malipo kutumia maeneo hayo.

“Kwa wale waliokuwa wakikodi maeneo haya kwa ajili ya shughuri za biashara au shughuri zingine, wataendelea kufanya hivyo kwa utaratibu wa manispaa na maeneo haya sasa yatakuwa chini ya uratibu wa manispaa,” alisema Mhere.

Aidha msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya ukandarasi ya Group Six International, Seleman Hamduni, alisema mradi huo utakamilika baada ya miezi miwili na katika ubora unahitajika.

“Katika eneo hili la Mwembeyanga ujenzi wa miundombinu ya maeneo haya ya wazi kama maeneo ya michezo, tumefikia asilimia 25 ya ujenzi wake, mkataba wa mradi huu ni miezi miwili na utakamilika kwa wakati,”alisema Hamduni.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea eneo la Mwembeyanga, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mwegelo, alisema mradi huo ni sehemu ya mipango ya jiji la Dar es Salaam la kuboresha maeneo yake na kuyafanya kuwa ya kijani.

Joketi alisema mradi huo ukikamilika Manispaa ya Temeke itapendeza na kuvutia watu kutoka katika maeneo mengine.

“Mradi huu unaenda kuibadilisha Temeke tunaenda kupanda miti na maua kwenye Mfereji wa Serengeti na kandokando ya barabara ya Mtoni Kijichi kuelekea Toangoma.

Mkuu huyo wa wilaya alisema miti 500 watapewa wananchi kwenda kupanda kwenye maeneo yao, ili nao washiriki kampeni ya ja Dar ya kijani.

Alisema Manispaa ya Temeke inatekeleza wa vitendo maagizo ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos ya Makala ya kutaka Jiji kuwa Safi na maeneo ya wazi ya kuwa ya kisasa na yenye mvuto.

Joketi alisema kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka utunzaji wa mazingira inatekelezwa kwa vitendo wilayani hapo na kwamba hawatamuangusha.

“Nawaomba wananchi wa maeneo ya jirani kujitokeza kushiriki ujenzi wa miundombinu ya kisasa, lakini pia muwe watunzaji wa maeneo hayo,” alisema.

Mwisho
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages