Breaking

Thursday 21 July 2022

TMA YATOA TAHADHARI MVUA ZINAZOENDELEA



Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imewataka watu wote kuendelea kuchukua tahadhari kuhusu na ushauri na utabiri unaotolewa na TMA ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza.

Rai hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Mtaalamu na Mchambuzi wa Hali ya Hewa kutoka kitengo kikuu cha Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Rose Senyagwa wakati akizungumzia mvua zinazondelea nchini hususani katika maeneo ya ukanda wa Pwani.

Amesema kuwa, mvua zinazoendea katika ukanda huo pamoja na baadhi ya maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki zimesababishwa na upepo wenye unyevuunyevu unaovuma kutoka bahari ya hindi kueleka katika maeneo ya nchi yetu na hivyo kusukuma unyeunyevu huo.

"Mvua zinazoendelea katika maeneo ya ukanda wa Pwani nikimaanisha Mikoa ya Tanga,Dar es salaam,Pwani,Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro,lindi Mtwara,Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na baadhi ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki mikoa ya Kilimanjaro,Arusha na Manyara zimesababishwa na upepo wenye unyevuunyevu unaovuma kutoka bahari ya hindi"amesema Senyagwa

Amesema kuwa ni vyema katika kipindi hicho cha baridi na Upepo mkali wananchi wakazingatia tahadhari zinazotolewa kwa kujikinga ili kujihadhari na madhara ya kiafya.

"Nyakati ambazo kuna ukungu mzito barabarani madereva wanapaswa kuwa makini wanapoendesha magari kwani inapunguza uono wa kuoa umbali mrefu hivyo wanashauriwa kuzingatia na kuchukua tahadhari" amesema Senyagwa

Aidha, amesema mvua hizo zilianza mwezi Juni katika kipindi cha Kipupwe na zimekuwa zikijitokeza kwa mvua za kawaida hivyo wameziita mvua za nje ya msimu na wanatarajia zitaendelea kuwepo katika kipindi cha Mwezi July mpaka Agosti mwaka huu.


Ameongeza kuwa kutokana na utabiri wa msimu wa kipupwe ambao ulitolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa mwishoni mwa mwezi Mei maeneo mengi ya nchi yalitarajiwa kuwa na vipindi vya baridi na upepo mkali.

Hata hivyo, amesema katika maeneo ya ukanda wa Pwani na Maziwa Makuu vipindi vya upepo mkali bado vinatarajiwa kuendelea kujitokeza upepo unaofikia Kilomita 40 au kuzidi kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofika mita mbili yanatarajiwa kuendelea kujitokeza.

Aidha, wamewashauri wananchi wanaofanbya shughuli zao kuendelea kuchukua tahadhari kipindi cha upepo mkali ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages