Breaking

Monday 1 August 2022

SIMBA SC YALAMBA BILIONI 26.1 MKATABA NA M-BET



Na Said Muhibu

Klabu ya ligi kuu Tanzania bara (NBC) Simba Sports Club imetangaza rasmi thamani ya mkataba wao uliosaniwa baina yao na kampuni ya michezo ya kubashiri M-Bet ambayo kiasi cha Bilioni 26, Milioni 168 na shilingi 5,000 kwa miaka mitano.

Thamani ya mkataba huo imetangazwa leo na Mkurugenzi wa Masoko M-Bet Allen Mushi kwenye ufunguzi wa wiki ya Simba kuelekea Simba Day mnamo Agosti 8, 2022.

Ndugu Mushi ameainisha kiwango cha fedha za udhamini kwa kila mwaka ambapo mwaka wa kwanza ni Bilioni 4.670, mwaka wa pili Bilioni 4.925, mwaka wa tatu Bilioni 5. 205, mwaka wa nne Bilioni 5.514 na mwaka wa tano Bilioni 5.583 ambayo jumla inakuwa Bilioni 26, Milioni 168 na shilingi 5,000.

Simba ilitangaza kuingia mkataba na M-Bet wa kuidhamini klabu hiyo kwa miaka mitano Julai 1, 2022 pasi na kutaja kiwango cha thamani ya mkataba huo.

Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi klabu ya Simba Salim Abdallah amewapongeza M-Bet kwa udhamini huo na kuwaahidi makubwa ndani ya kipindi watakachokuwa wameidhamini klabu hiyo.

"Sisi Simba ni waungwana, tunawashukuru wadhamini waliopita, sasa tupo na mdhamini mpya na tunaamini tutafanya kazi kwa karibu," alisema.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages