Breaking

Friday 18 November 2022

DAWA ZA KULEVYA ZAMUIBUA ASKOFU MWAMALANGA


Na Mwandishi Wetu

MWENYEKITI wa Kamati ya Kitaifa ya Maaskofu na Mashekhe ya Maadili Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini nchini, Askofu William Mwamalanga ameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kuwataja wahadharani watu wanaodaiwa kujishughulisha na biashara hiyo haramu.

Askofu Mwamalanga ametoa pongezi hizo siku chache baada ya Kamishina Mkuu wa DCEA, Gerlad Kusaya kujitokeza mbele ya vyombo vya habari na kuwataja hadharani watuhumiwa wa dawa za kulevya tisa ambapo wanadaiwa kukutwa na kilo 34.89 ya heroine jijijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Waliokamatwa ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Dar es Salaam, Kambi Zuberi Seif, Muharami Sultan (40) na John John, maarufu Chipanda (40) ambaye jukumu lake ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka kwenye kituo hicho.



Wengine ni Said Matwiko, mkazi wa Magole, Maulid Mzungu maarufu Mbonde (54) mkazi wa Kisemvule, Rajabu Dhahabu (32) mkazi wa Tabata, Seleman Matola Said (24), mkazi wa Temeke Wailes, Hussein Pazi (24) mfanyabiashara na Ramadhani Chalamila (27) mkazi wa Kongowe.

“Sisi viongozi wa dini tunaona huu ni ushindi mkubwa kuwahi kutokea hongera sana mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya nchini kwani kwa muda mrefu sasa Watanzania wamekuwa wakipiga kelele juu ya kuibuka upya biashara hiyo haramu,” alisema

Mwamalanga alisema kuibuka kwa biashara hiyo kumekuwa kukihusihwa na vyombo vya michezo na baadhi ya madhehebu ya dini, hivyo kuishauri mamlaka hiyo kuongeza nguvu katika mapambano.

Alisema miaka ya nyuma viongozi wa dini wakiwamo Mashekhe na Maaskofu walitoa orodha ndefu ya waingizaji wakubwa wa dawa za kulevya nchini, lakini hakikufanyika chochote.

“Ndiyo maana tuipongeza mamlaka hii kwa kuthubutu. Hakika tukuombea dua ya ulinzi Kamishna Kusaya kwa Mwenyezi Mungu aendelee kukupa ulizni wa kufanya kazi yako kwa weledi, katika kulilinda Taifa dhidi ya dawa za kulevya....

Tunahimiza viongozi wakuu wa michezo nchini kujisafisha na kusafisha timu zao ili zisitumike na wahalifu wachache kuliangamiza Taifa kwa tamaa zao za utajiri wa haraka bila baraka,” alisema.

Aidha, Askofu Mwamalanga alisema wanamuomba Kamishna Kusaya kuisafisha mamlaka hiyo kwa kuwaondoa baadhi ya watendaji ambao wanatajwa kuficha wahalifu pindi wanapowakamata kwa kupewa rushwa kubwa za magari na pesa.

“Ni vema chombo kikafanya kazi zake kwa uwazi, bila kulinda wahalifu wanaotumia dini na michezo kusafirisha dawa za kulevya...sisi tumejipa jukumu la kukemea na kutoa ushirikiano wa kila siku kwa mamlaka, ili Tanzania bila dawa za kulevya isomeke kwa vitendo,” alisisitiza.

Mwisho
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages