Breaking

Friday 18 November 2022

DC KYERWA APIGA MARUFUKU SHUGHULI ZA KIBINADAMU KARIBU NA VYANZO VYA MAJI



Na Lydia Lugakila, Kagera

Katika hali ya kuendelea kutunza mazingira shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji zimeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kuharibu mazingira.

Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilicholenga kujadili taarifa za robo ya kwanza 2022/2023 katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kyerwa Mkuu wa wilaya hiyo Rashid Mwaimu amesema kuwa hayupo tayari kuona au kusikia uharibifu wa mazingira badala yake shughuli zote za upandaji miti zifanyike kitaalam ili kutunza mazingira.

Amesema kuwa vyanzo vya maji vikiwemo mito maziwa viendelee kutunzwa na shughuli hizo kusitishwa mara moja.

"Nakuagiza mkurugenzi tuhakikisha zoezi la upandaji wa miti ndani ya mita 60 lifanyike ili kutunza mazingira ukataji miti ovyo ukome"alisema Mwaimu.

Ameongeza kuwa tayari ameunda timu maalum ambayo itapita kwenye vyanzo vya maji ambayo itakaa na watu kutoka hifadhi ya misitu ili kuona namna ya utunzaji wa vyanzo hivyo.

Aidha amewaomba wananchi wilayani humo kutumia vyema mvua zinazonyesha kwa kuhakikisha wanapanda mazao ya chakula na biashara, yanayohimili ukame ikiwa ni pamoja na kuweka akiba ya chakula.

Hata hivyo amehimiza kutilia maanani suala la lishe ili kuzalisha kizazi kisicho na udumavu huku akiwataka madiwani hao kuendelea kutoa elimu ya lishe katika jamii.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages