Breaking

Thursday 17 November 2022

KATIBU MKUU MADINI ASISITIZA MRADI WA GRAPHITE MAHENGE KUHARAKISHWA




Katibu Mkuu Wizara ya Madini Adolf Ndunguru amehimiza kupatiwa ufumbuzi na kutatuliwa changamoto zinazoukabili Mgodi wa uchimbaji wa Madini ya Kinywe wa Mahenge unaomilikiwa na Kampuni ya ubia ya Faru Graphite Corporation ili uzalishaji wa madini hayo ya kimkakati duniani uanze nchini.

Amesema hayo Novemba 16, 2022 Jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Wadau wezeshi wa Mgodi wa Mahenge Graphite uliolenga kuwezesha ujenzi wa miundombinu muhimu ili kufanikisha kuanza kwa mradi wa uchimbaji wa madini ya Kinywe.

Ndunguru amesisitiza kuanza ujenzi wa barabara zinazofaa kutoka Ifakara hadi eneo la mgodi na upatikanaji wa usafiri wa reli kwa ajili kupeleka madini kutoka Ifakara hadi Bandari ya Dar es salaam.

Pia, ametaka kufikishwa kwa nishati ya umeme katila eneo la mgodi kwa ajili ya kupata nishati. Aidha, amesisitiza upatikanaji wa maeneo ya ardhi karibu na reli ya TAZARA Ifakara pamoja na kutoa msaada kuwezesha zoezi la makazi mapya na ulipaji wa fidia.

Ameongeza kuwa, ujenzi wa miundombinu hiyo utasaidia katika maendeleo ya mgodi na jamii zinazozunguka mgodi ili uwe na manufaa.

"Katika kikao hiki na kama nilivyoeleza, tunao wadau muhimu kwa pamoja tukiwa na lengo la kuhakikisha mradi wa madini ya Kinywe unaanza kufanya uzalishaji kwa kuwa una tija kubwa sana kwetu kama Serikali na wawekezaji," amesema Ndunguru.

Naye, Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Musa Ali Mussa amesema kuanza kwa mradi huo kutawezesha kuongeza mapato kwa Serikali na kutoa ajira kwa Watanzania ikiwemo fursa fursa mbalimbali katika mgodi huo.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wadau wa Sekta ya Madini wakiwemo TAZARA, TPA, TANROADS, TARURA, Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Wizara ya Kazi, TANESCO na TANAPA.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages