Breaking

Sunday 6 November 2022

KIKWETE ATAKA SERIKALI KULINDA HAKI ZA WASANII, AIPONGEZA WIZARA KUKUZA SEKTA YA SANAA



Na John Mapepele

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kazi kubwa inayoifanya ambayo imesababisha kuwa miongoni mwa sekta zinazokuwa kwa kasi na kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Mhe. Kikwete ameyasema haya Usiku wa kuamkia leo Novemba 6, 2022 akiwa Mgeni wa rasmi kwenye uzinduzi wa albamu ya Ommy Dimpoz iitwayo Dedication mara baada ya kukaribishwa kutoa hotuba yake na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye amekuwa mgeni wa heshima kwenye uzinduzi huo.


Amefafanua kuwa katika awamu hii ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan tasnina ya muziki wa kizazi kipya imekua kwa kasi na kupata mafanikio makubwa ukilinganisha awamu zilizopita.

“Kila siku nikiangalia kwenye televisheni naona wanamuziki na wasanii wapya hali ambayo inaashiria kumekuwa na ukuaji wa kasi na kusababisha ajira kwa vijana” ameongeza Mhe. Kikwete.


Aidha, amesema changamoto iliyopo kwa sasa kwenye tasnia ya muziki ni namna gani ya kuhakikisha wanamuziki wanapata malipo kwa kazi zinazopigwa kwenye vyombo vya Habari na kusisitiza Serikali kupata ufumbuzi wa kudumu wa suala hili ili kuwasaidia wanamuziki waweze kunufaika na jasho la kazi zao.

Ametoa wito kwa Serikali kuendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa haki za wanamuziki zinalindwa kisheria ili wanamuziki waweze kufanikiwa huku akifafanua kuwa duniani kote wanamuziki na wasanii wanaongoza kwa kuwa na vipato vikubwa.


Amempongeza Mtendaji Mkuu mpya wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Dkt. Kedmon Mapana kwa kuteuliwa na Mhe. Rais kushika nafasi hiyo huku akimwelezea kuwa anauwezo na mchango mkubwa kwenye sekta ya Sanaa nchini na kumtaka kuendelea kutoa mchango huo kwa faida ya taifa la Tanzania.

Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akimkaribisha Rais mstaafu Kikwete ili aweze kutoa hotuba yake amesema Sekta ya Sanaa ndiyo sekta iliyoongoza kwa kasi ya ukuaji na kufafanua kuwa mwaka uliopita iliongoza kwa kukua ambapo ilikuwa kwa 19% na kwamba dhamira ya Serikali ni kutaka sekta hiyo kuendelea kukua kwa kasi ili iweze kuchangia kwenye uchumi wa nchi na kutoa ajira za uhakika kwa vijana.


Aidha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa na msukumo anaoutoa kwenye sekta hizo ambao umesaidia kuleta mafaniklio makubwa katika kipindi kifupi cha utawala wake, huku pia akimpongeza Mhe. Kikwete kwa kazi aliyoifanya ya kusaidia wasanii katika awamu yake.

“Mhe. Rais Mstaafu nina furaha ya kueleza kuwa sekta hizi ni sekta za kuleta furaha kwa wananchi na kwa kweli changamoto kwa sasa tunayoipata tunaweza kusema ni suala la kuongeza muda wa furaha, tungependa kuongeza muda wa furaha hasa kwenye majiji hapa nchini ili wananchi waendelee kufurahi” ameongeza Mhe. Mchengerwa


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages