Breaking

Thursday 10 November 2022

SERIKALI YAAGIZA UJENZI SHULE 232 ZA SEKONDARI KUKAMILIKA KWA WAKATI



Na Fred Kibano OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI Angellah Kairuki ametoa maagizo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya nchini kuhakikisha ujenzi wa miundombinu ya shule za Sekondari 232 unakamilika kwa wakati.

Waziri Kairuki ametoa kauli hiyo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa nne wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara, tarehe 09 Novemba, 2022 katika Ukumbi wa Masista wa Shirika la Ivrea Jijini Dodoma.

Waziri Kairuki amesema Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya Nchini wahakikishe ujenzi wa madarasa 8,000 yenye thamani ya shilingi milioni 470 kwa kila shule ya sekondari unakamilika kabla au ifikapo tarehe 15 Disemba, 2022 ili kuwezesha wanafunzi wote watakaofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi 2022 wanajiunga na Kidato cha kwanza Januari, 2023.




Aidha, amesema kupitia mwaka huu wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia mradi wa BOOST itajenga zaidi ya madarasa 9,000 nchini kote na kutoa rai kwa watendaji hao pindi mradi huo utakapofika katika maeneo yao kuhakikisha wanasimamia ujenzi na ukarabati wa shule za msingi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu ili Serikali iweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Serikali imezindua mradi mpya utakaotekelezwa kwa miaka 5 wa kuboresha upatikanaji wa fursa sawa katika ujifunzaji bora wa Elimu ya Awali na Msingi, Tanzania Bara (BOOST) kwa gharama ya shilingi 1.15 Trilioni, Mojawapo ya afua zitakazotekelezwa kupitia mradi huu ni ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika shule za Msingi zenye uhitaji mkubwa zaidi” amesema Kairuki.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages