Breaking

Tuesday 20 December 2022

WANAODAIWA KUWA MAJAMBAZI WAUA WAKALA



Mkazi wa Butengwa Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga Richard Nzumbe ambaye ni wakala wa huduma za fedha amefariki dunia baada ya kuvamiwa na na waodhaniwa kuwa majambazi na kupigwa Risasi akiwa anaingia nyumbani kwake akitokea kwenye duka lake la huduma za fedha.

Tukio hilo la uvamizi kwa kutumia silaha uliosababisha kifo cha Richald Nzumbe,limetokea Desemba 19,2022 majira ya saa 1 usiku katika Kata ya Butengwa Manispaa ya Shinyanga Mkoani humo.

Akieleza juu ya tukio hilo Mwenyekiti wa Mtaa Butengwa,Onesmo Mayeba,Amesema majira ya saa 1 usiku alipewa taarifa na mwananchi juu ya tukio hilo ambapo alifika eneo husika na kukuta majambazi hao wamekwisha tenda uvamizi huo huku ikisemekana lengo la kufanya uvamizi huo ni kuwania fedha kutoka kwa marehemu Richald.

“Tukio hili ni lakikatili na tunalilaani kwa sababu majambazi hawa wametoa uhai wa mtu ambapo ni kosa la jinai,hivyo tunaliomba jeshi la polisi kuwabainisha wote waliohusika kutenda mauaji hayo na kuwapa adhabu kulingana na Sheria”Amesema Mayenda.

Awali akieleza undani wa tukio hilo Shemeji wa marehemu,Salome Dady, amesema majira ya saa 1 usiku walikuwa ndani yeye na watoto wa dada yake,ndipo waliposikia gari la shemeji yake likiwa limefika getini ambapo mtoto wake alienda kufungua geti hilo ndipo aliposukumwa na majambazi hao na kumfuata marehemu kisha kumfanyia unyama huo.

"Tulikuwa ndani mimi na watoto wa dada mara tukasikia gari likiwa getini ambapo alienda mtoto wa dada kufungua mlango ndipo nikasikia kelele nje ikabidi nitoke nikaone kuna nini nikakuta watu wawili wanampiga risasi shemeji ikabidi nichukue stuli nikampiga mmoja akaanguka alafu nikaenda kuchukua kisu nikamchoma nacho mwingine ndo wakachukuana wakaondoka"Amesema Salome Dady.

Aidha Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Shinyanga,ACP,Janeth Magomi Amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema Jeshi la polisi linaendelea na msako wa kina kuwabainisha waliohusika na tukio hilo.


Via: Huheso Digital
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages