Breaking

Wednesday 1 March 2023

RC BATILDA AONYA MAKAMPUNI YA TUMBAKU YASIYOLIPA WAKULIMA



Na Lucas Raphael,Tabora


MAKAMPUNI ya wazawa na ya kigeni yanayojishughulisha na ununuzi wa zao la tumbaku Mkoani Tabora yametakiwa kulipa kiasi cha shilingi bil 1.6 za mavuno ya msimu uliopita vinginevyo yatafikishwa mahakamani na kutaifishwa mali zao ili kuweza kufidia kiasi gharama kwa  (Amcos).

Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 5 wa mwaka wa Chama Kikuu cha Ushirika Milambo uliofanyika jana Wilayani Kaliua.

Alisema kwamba kampuni hizo zitafikishwa mahakamani na kuifishwa mali zao kwani wanaonekani wazi hawataki kulipa madai ya wakulima jambo ambalo serikali ya mkoa  hawalikubali bali mkono wa sheria ndio utaamua.

‘Kampuni yoyote ambayo haijamaliza kulipa madeni ya wakulima ya msimu uliopita ilipe haraka iwezekanavyo, la sivyo tutawafikisha mahakamani, haiwezekani uchukue tumbaku ya mkulima halafu usimlipe’, alisema

Alisema kwamba wakulima wamekuwa wavumilivu hivyo serikali ya mkoa inalibeba jambo hilo ili wakulima waweze kupata haki yao ya msingi.

Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa  wa Tabora aliyataka makampuni ya ununuzi wa zao la kutumbaku mkoani hapa kuhakikisha yalipa madeni yao yote ya nyuma kabla ya kuanza msimu mpya wa masoko ya zao hilo mwaka huu.

Alisema licha ya baadhi ya makampuni kumaliza madeni yao hadi sasa baadhi ya vyama vya msingi (Amcos) havijalipwa zaidi ya sh bil 1.6 za mavuno ya msimu uliopita na sasa tumbaku imeiva na msimu mpya wa masoko unakaribia kuanza. 

Balozi Dkt Batilda alibainisha kuwa kilimo cha tumbaku ni kazi ngumu inayohitaji kujituma na uangalizi wa karibu sana na usipohudumia vizuri shamba lako huwezi kupata tumbaku nzuri yenye ubora unaotakiwa katika soko la dunia na yenye gredi ya juu.

Alisisitiza kuwa serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kufanya juhudi kubwa za kuboresha shughuli za wakulima ikiwemo kutoa ruzuku ya pembejeo, na kutafuta wanunuzi wakubwa ili tumbaku yote inayozalishwa inunuliwe.

Balozi Batilda alifafanua kuwa katika msimu uliopita pekee jumla ya kilo mil 30 za tumbaku zilizalishwa na wakulima na kuuzwa zote na kwa mwaka huu makisio yao ni kuzalisha kilo mil 60 na zitauzwa zote tena kwa bei nzuri.

Alitoa wito kwa viongozi wa Ushirika na Amcos kuendelea kuhamasisha suala zima la upandaji miti katika maeneo yao na kuhakikisha miti inayopandwa inaendana na ardhi ya eneo husika kwa kuwa baadhi ya miti huathiri mazingira.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa waTabora, Hassan Wakasuvi aliwataka viongozi wa Ushirika kuwa watetezi wa kweli wa wakulima na kutowaibia fedha zao.

Alishauri wakulima kutunza vizuri tumbaku yao na kuifunga vizuri katika mabelo baada ya kuvunwa ili ikienda sokoni isitolewe kasoro yoyote, ipendwe na makampuni yote na kuuzwa kwa bei nzuri.

‘Viongozi wa vyama vya msingi shirikianeni, pendaneni, watendeeni wema wanachama wenu, acheni kuwaibia wanachama wenu, alichokopa mkulima ndicho alipe si vinginevyo’, alisema.

Alisisitiza kuwa Chama Cha Ushirika Milambo kilipaswa kuwa juu zaidi kuliko hata vyama vingine vilivyoko katika Mkoa huo vya WETCU na IGEMBENSABO kwa kuwa kinazalisha kilo nyingi za zao hilo na mazao mengine.

Mbunge wa Jimbo la Kaliua Aloyse Kwezi alisema kwa mwaka jana pekee Wilaya yake ya Kaliua ilizalisha zaidi ya kilo mil 20 za tumbaku kuliko wilaya nyingine lakini akasikitishwa na tabia ya baadhi ya wanunuzi kutolipa kwa wakati.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages