Breaking

Wednesday 1 March 2023

MADAKTARI FEKI WAKAMATWA MUHIMBILI

 

Hospitali ya Taifa Muhimbili imewakamata madaktari feki wawili waliojitambulisha kwa jina la Josephat Joseph na Khamis Hamad Bakari baada ya uongozi wa hospitali hiyo kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano Hospitali ya Taifa Muhimbili Februari 28 2023 imeeleza kuwa Watuhumiwa hao wamedaiwa kuwahadaa wagonjwa na ndugu zao kuwa wao ni madaktari na kutumia mwanya huo kujipatia fedha isivyo halali, ambapo uongozi uliweka mtego baada ya kupata taarifa hizo na kufanikiwa kuwakamata.

Josephat Joseph amekamatwa katika kliniki ya magonjwa ya Ngozi Februari 27, mwaka huu huku Hamis Hamad Bakari ambaye alikuwa akishirikiana naye alikamatwa maeneo ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).

Watuhumiwa hao wamefikishwa katika Kituo Kikuu cha Kati kilichopo jjini Dar es Salaam kwa ajili ya hatua za kisheria.

Aidha, hospitali imetoa rai kwa wananchi kuchukua tahadhari ikiwemo kutoa taarifa kwa uongozi wa hospitalli pale wanapomtilia shaka mtoa huduma ili kuepuka watu wenye nia ovu kama hao na kuwaelekeza watumishi wa hospitali hiyo kuvaa vitambulisho muda wote wa kazi ili jamii iweze
kuwatambua kwa urahisi.

"Pia tunawakumbusha wananchi kwamba malipo yote ya hospitali yanafanyika kupitia kumbukumbu namba (control number) ambapo ukilipia huduma, jina la Hospitali ya Taifa Muhimbili litatokea" imeeleza taarifa kutoka uongozi wa Muhimbilli.

 
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages