Breaking

Monday 27 March 2023

ZIARA YA RAIS SAMIA AFRIKA KUSINI YALETA MATOKEO CHANYA SEKTA YA MADINI


*Zaidi ya wawekezaji 30 kutoka Afrika Kusini wameingia nchini*


*Wamepongeza marekebisho ya Sheria yaliyofanyika sekta ya Madini*


Baada ya ziara  ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan  aliyoifanya hivi karibuni nchini Afrika Kusini, ujumbe wa Wawekezaji zaidi ya 30 kutoka nchi hiyo wamekutana na Wizara ya Madini pamoja na Taasisi zake kwa lengo la kupata uelewa wa mazingira ya uwekezaji nchini.


Katika kikao kilichowakutanisha wataalamu kutoka Wizara ya Madini pamoja na Taasisi zake, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amewashauri wawekezaji hao kuwekeza kwenye shughuli za Madini ikiwemo Uchimbaji wa Madini,  Uongezaji Thamani Madini na uuzaji wa vifaa vya shughuli za madini.


Akiwasilisha mada kwa wawekezaji hao, Dkt. Mwanga amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na Madini ya aina mbalimbali yakiwemo Madini ya kimkakati ambayo kwa sasa dunia inayahitaji kwa kiwango kikubwa kwa ajili ya maendeleo ya teknolojia ambapo amewakaribisha kuwekeza nchini ili pande zote ziweze kunufaika na uwepo wa Madini hayo.


Pamoja na mambo mengine, Dkt. Mwanga amewapongeza wawekezaji hao kwa kufika nchini ili kupata maelezo na kujifunza mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania na amewaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha shughuli za uwekezaji nchini.


Pia, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imetumia fursa hiyo kuwasilisha mada juu ya uwepo wa Madini na kiwango cha Madini kilichopo katika maeneo mbalimbali ya nchi pamoja na jiografia ya Tanzania.


Katika hatua nyingine, Afisa Masoko Mark Stephano kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) amewasilisha mada kwa wawekezaji hao ambapo amesema shirika hilo lipo tayari kuungana na mwekezaji yeyote kutoka ndani au nje ya nchi ili kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kunufaisha pande zote mbili.


Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe huo Roelof Tonder amesema Afrika  Kusini imeanza shughuli za Madini miaka mingi iliyopita hivyo, imefarijika kuona Tanzania imefanya marekebisho makubwa kwenye Sheria ya Madini ambayo yanalenga kuinufaisha nchi pamoja na Wananchi.


Tonder amesema ujumbe uliyofika nchini Tanzania unatamani kuwekeza katika maeneo tofauti hususan kwenye sekta ya Madini ambapo amesema Ujumbe umefurahishwa na hali nzuri ya utulivu wa Kisiasa uliyopo nchini humo.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages