Breaking

Tuesday 13 June 2023

TBS KUPITIA MRADI WA TANIPAC YATOA MAFUNZO YA SUMUKUVU WILAYANI KITETO,KONGWA,GAIRO,KILOSA

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kutoa mafunzo ya udhibiti wa sumukuvu kwenye mahindi, karanga na bidhaa zake katika wilaya za Kiteto, Kongwa,Gairo na Kilosa ambapo yamewafikia wasafirishaji,wafanyabiashara na wasindikaji wa mahindi na karanga zaidi ya 600.

Mafunzo hayo ambayo yalianza kutolewa na TBS kwenye wilaya hizo kuanzia Mei 31, mwaka huu yakitarajiwa kuhitimishwa Juni 14, mwaka huu yanatolewa na shirika hilo kupitia Mradi wa Kitaifa wa Kudhibiti Sumukuvu ujulikanao kama Tanzania Initiative for Preventing Aflatoxin Contamination (TANIPAC).

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo hayo Bw.Jabir Abdi Mwenyekiti wa mradi huo TBS alisema mafunzo hayo yatawasadia wasafirishaji,wafanyabiashara na wasindikaji wa mahindi na karanga kuweza kupata masoko ya uhakika na kuwezesha wananchi kuepukana na madhara ya kiafya yatokanayo na sumukuvu.

Bw. Abdi alitaja faida za mafunzo kuwa yalenga kulinda afya za binadamu, kuwezesha biashara ya mazao ya mahindi na karanga, kulinda afya za mifugo na kuwezesha utoshelevu wa chakula salama.

Kwa mujibu wa Bw.Abdi faida nyingine za mafunzo hiyo ni kuwawezesha wadau katika mnyororo wa karanga, mahindi na bidhaa zake kuhimili ushindani katika masoko ya ndani, kikanda na nje ya nchi.

Alisema sumukuvu huathiri zaidi mazao ya mahindi na karanga ambayo ni sehemu muhimu ya chakula cha Watanzania hapa nchini.

"Kwa sababu hiyo sisi sote tunatakiwa kuzingatia mikakati ya kukabiliana na sumukuvu ili vyakula vyetu viendelee kuwa salama kwa muda wote," alisisitiza Bw Abdi.

Alifafanua kwamba TBS inatambua nafasi ya wafanyabiashara, wasindikaji na wasafirishaji kwa ujumla na mchango walionao, hivyo TANIPAC imeandaa mafunzo hayo mahususi kupitia TBS ili kuwajengea uwezo kwa ajili ya udhibiti sumukuvu.

Alihimiza wadau hao kuzingatia mambo muhimu yanayoshauriwa na wataalam ili kudhibiti sumukuvu katika chakula, ikiwa ni pamoja na kuzingatia kanuni bora za kilimo kama inavyoshauriwa na wataalam, kuvuna na kuondoa shambani mahindi na karanga mara baada ya kukomaa vizuri na kukaushia vizuri mazao yaliyovunwa kabla kuhifadhi.

Nyingine ni kuepuka kurundika mazao moja kwa moja kwenye sakafu, kuhakikisha wanahifadhi vizuri mazao kwa lengo la kuepuka wadudu waharibifu, wanyama, joto kali na unyevunyevu.


Baadhi ya Washiriki wa mafunzo ya udhibiti wa sumukuvu kwenye mahindi na karanga pamoja na bidhaa zake wilayani Gairo mkoa wa Morogoro
Washiriki wa mafunzo ya udhibiti wa sumukuvu kwenye mahindi na karanga pamoja na bidhaa zake wilayani Kongwa wakijifunza namna ya kutumia kipima unyevu.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Bw.Shaka Hamdu Shaka akifungua mafunzo ya udhibiti wa sumukuvu kwenye mahindi na karanga pamoja na bidhaa zake katika ukumbi wa Triple S wilayani Kilosa.
Washiriki wa mafunzo ya udhibiti wa sumukuvu kwenye mahindi na karanga pamoja na bidhaa zake wilayani Kiteto wakifuatilia mafunzo

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages